
LEO ni Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) ambapo staa mpya wa kike nchini Tanzania, Zuchu ametangaza kuwa usiku wa leo atakuwa na jambo kubwa katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Pamoja na shoo ya Valentine, lakini mashabiki wengi wanasubiria kwa hamu huku baadhi yao wakibashiri kuwa huwenda akachumbia na mwanaume ambaye si mwingine bali ni bosi wake, Diamond Platnumz.
Hii ni kutokana na uvumi ambao umekuwepo juu ya wawili hao kuwa ni wachumba kwa muda mrefu sasa.
Tayari upande wa mama mzazi wa Zuchu, Bi Khadija amezungumza akisema hakuna ubaya kwani wawili hao siyo wazaliwa wa tumbo moja.
Hata hivyo, habari za ndani zinasema kuwa, mtu pekee ambaye ametia ngumu juu ya kuwepo kwa ndoa ya Diamond na Zuchu ni mama mzazi wa jamaa huyo, Mama Dangote ambaye hataki kabisa kusikia jambo kama hilo na ukumbuke yeye ndiye ‘last say’ (mwamuziki wa mwisho) kwenye jambo lolote linalomhusu mwanawe huyo.
Wiki mbili zilizopita, Zuchu alitangaza kuwa atafanya jambo kubwa siku hii ya Wapendanao ambalo inasemekana ni kuchumbiwa.
Chanzo kutoka ndani ya familia ya Diamond au Mondi kimedai kwamba, kuna shinikizo kubwa kwa jamaa huyo kutoka kwa baadhi ya ndugu ambao wanamtaka amuoe Zuchu, lakini mtu pekee ambaye hataki kusikia jambo kama hilo ni Mama Dangote.
Mama Dangote anadaiwa kuchukizwa mno na taarifa au shinikizo hilo la Diamond kutakiwa amuoe Zuchu.
Vuguvugu la Diamond na Zuchu kuwa ni wapenzi lilianza kitambo mno, lilianza muda mfupi tu baada siku ile ya Aprili 8, 2020, pale mrembo huyo aliposainiwa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya Diamond.
Baada ya hapo, wawili hao wamekuwa na vipindi tofauti vya kupanda na kushuka, lakini hivi karibuni ishara zimekuwa ni nyingi mno huku wakipostiana kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya ndugu kumsifia Zuchu kuwa anafaa kuwa mkewe Diamond.
Katika hali inayoonesha kuwa mashabiki wa Diamond wanaipenda ‘kapo’ yake na Zuchu, mara kadhaa wamekuwa wakishabikia na kuwasifia wanapowaona wawili kwenye picha ya pamoja.
Wawili hao wamekuwa wakiibua shangwe kama lote mitandaoni kwa upande wa mashabiki wao na inapotokea mmoja akasema hawaendani, basi anakuwa amesababisha uvunjifu wa amani, kwani anakuwa amewakata stimu na kuishia kuoga matusi ya nguoni.
Hata hivyo, gazeti hili lilipozungumza na Esma; dada wa Diamond kuhusu kinachoendelea kwa wawili hao, alisema; “Naomba mniweke mbali kabisa na jambo hilo, safari hii sitaki kabisa kuhusishwa na wifi yangu maana nimeshapewa majina ya kila aina kwa sababu ya mawifi…”
Hata hivyo, mara kadhaa Diamond na Zuchu wamekuwa wakikanusha kwa nguvu kubwa kuwa, hawana uhusiano wa kimapenzi, kwani wanaheshimiana kama mtu na bosi wake au mtu na kaka yake.
“Ninamheshimu sana Diamond kama bosi wangu na hajawahi kunikosea heshima,” anasema Zuchu.
Zuchu ni msanii wa pili wa kike kusainiwa Wasafi baada ya dada yake Diamond kwa baba mmoja, Queen Darleen.
Tangu Zuchu asajiliwe, amekuwa akipewa kipaumbele kimuziki na Diamond, jambo ambalo limezua maswali na wengine kumsihi Zuchu kuwa makini, asije akaingia kwenye himaya ya mapenzi ya msanii huyo, kwani mwisho wake hautakuwa mzuri.
STORI; SIFAEL PAUL, DAR