
FAMILIA ya mwanadada Muna Love ambaye inasemekana kuwa hali yake ni mbaya baada ya upasuaji (sajari) wa kurekebisha maumbile ya mwili wake aliofanyiwa ‘kudunda’, imesema haina taarifa zozote kuhusu maendeleo ya afya yake.
Muna Love ambaye ni mwigizaji wa Bongo Movies na Mtumishi wa Mungu kama ambavyo mwenyewe amekuwa akijinasibu, amekuwa akilitafuta umbo la ndoto zake kwa kufanya upasuaji mara kadhaa kwa ajili ya kutafuta mwonekano bomba anaoutaka.
Hata hivyo, hivi karibuni alishtua wengi baada ya kusema kuwa anaijutia nafsi yake kwa kufanya ‘sajari’ na kutubu kwa Mungu wake akiwaomba Watanzania wasijaribu kufanya hivyo kwani ni hatari.
Kwa mujibu wa dada wa Muna Love ambaye ameomba hifadhi ya jina lake, wao kama familia hawajui anaendeleaje kiafya baada ya kutangaza kuwa na hali mbaya.
“Kwa kweli hatujui maana sisi hajatuambia kama anaumwa na hiyo sajari aliyoifanya hakutushirikisha kwa hiyo kuhusu mambo yake sisi kama familia hatujui lolote labda muwaulize rafiki zake.
Pia dada huyo akaibua madai mengine ya muda mrefu kwamba Muna Love aliikataa familia yake hivyo wao hawamtambui.
“… Wala hatukumkosea, naona alivyopata pesa akaona labda hatuna hadhi ya kuwa naye kwa hiyo akaamua kutukataa. Tunachojua muda utaongea, pesa zikiisha atatukumbuka, kwa sasa haoni umuhimu, lakini sisi ndiyo tutakaomlilia na kumzika,” alihitimisha ndugu yake huyo.
Baadhi ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakimtabiria mambo mabaya kwa madai kwamba, mambo hayo anayoyafanya ni kama anamkosoa Mungu wake na ndiyo yatakuwa mwanzo wa matatizo makubwa kwenye maisha yake.
STORI; MWANDISHI WETU, DAR