
Wakazi wa Kaunti ya Vihiga Magharibi mwa Kenya, walipigwa na butwaa baada ya kumuona kijana mwenye umri wa miaka 19, mikono yake ikiwa imepigiliwa misumari kwenye mti kwa madai ya wizi wa redio.
Polisi nchini Kenya sasa wameanza msako wa kumtafuta mtuhumiwa aliyefanya tukio hilo la kumpigilia misumari mvulana huyo kwenye mti.
Kulingana na ripoti ya polisi, Collins Sambaya alikutwa akiwa amepigiliwa mikono yake miwili kwenye tawi moja la mti kwa misumari.
“Tulipokea ripoti kutoka kwa chifu wa eneo la Izava Kaskazini, Evans Endesha kwa njia ya simu, akisema kuna watu walimpigilia misumari mtu mmoja kwenye mti,” ripoti ya polisi ilisema.
Maafisa wa polisi walifika kwenye eneo la tukio na kumkuta Collins akiwa bado kwenye mti lakini mtuhimiwa alikuwa ametoweka akikwepa kukamatwa.
Ripoti ya polisi iliongeza kuwa, “Wakati polisi walipokuwa wakikaribia eneo la tukio, mtuhumiwa huyo alitimua mbio na bado wanaendelea kumtafuta.”