
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Nchi ya Marekani katika sekta zote za maendeleo ili kusaidia kuongeza fursa za uwekezaji na biashara.
Ameyasema hayo Jumatano, Februari 23, 2022 alipozungumza na wabunge wa Bunge la Marekani Katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu amesema kuwa wabunge hao wamefurahi kuona mahusiano kati ya nchi hizi mbili yanakua.
“Mahusiano yetu kiuchumi yanaendelea kuimarika, wanatambua mchango wa Tanzania katika kutoa fursa za uwekezaji hapa Tanzania na sisi kufanya nao biashara, tutaendelea kuimarisha kwa kuwa na ‘forum’ mbalimbali za wafanyabishara wa ndani ya Nchi na Wamarekani.”
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuifungua Tanzania kimataifa katika maeneo mbalimbali ili kuongeza fursa kwa Watanzania.

“Mheshimiwa Rais ameelekeza tufanye mapitio na maboresho ya uwekezji na biashara, kwa kupitia sheria zetu na kuondoa maeneo ambayo yanakwaza wafanyabishara na kujenga uwezo kwa Watanzania kufanya biashara nje ya nchi, lengo ni kuinua uchumi na kufungua fursa za ajira kwa vijana wetu”
Amesema kuwa wabunge hao wameahidi kushirikiana na Tanzania katika mpango wa kuinua uchumi katika meneo mbalimbali kupitia miradi na programu mbalimbali kupitia taasisi za kimarekani.