×

Mabomu Ya Vacuum Tishio Ukraine

 


SIKU chache zilizopita, Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa, Oksana Markarova aliilalamikia Urusi kuwa inatumia mabomu hatari ya vacuum au thermobaric ambayo jamii za kimataifa ziliyapiga marufuku kutumika vitani.

 

Hii ni aina ya mabomu hatari na yenye madhara makubwa kwenye uwanja wa vita; wenyewe wanayaita ”Father of all bombs” yaani baba wa mabomu yote.

 

Mabomu haya yakitumika huweza kuleta maafa ya halaiki; ingawa vita haichagui silaha lakini nchi itakayotumia huweza kufikishwa kwenye mahakama ya uhalifu wa kivita.

 

Inaelezwa kuwa bomu la vacuum likifyatuliwa hutoa aina fulani ya mafuta ambayo baadaye hutengeneza mvuke wenye mfano wa wingu zito lenye kupenya eneo lolote hata kwenye handaki au nyumba zilizofungwa.

 

Baada ya kutokea hali hiyo, mlipuko wake hutokea na kusababisha madhara makubwa ikiwemo kuunguza majengo na kuua binadamu.

 

Hakuna ushahidi kwa sasa kuhusu Urusi kutumia silaha hizi katika vita yake dhidi ya Ukraine lakini mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, Karim Khan amesema kuwa, mahakama yake itachunguza.

 

Ingawa Urusi inalalamikiwa katika hili lakini silaha hizi zimewahi kutumiwa na Marekani kwenye vita yake na kundi la Al-Qaeda la Afghanistan katika kuziangamiza ngome za waasi waliokuwa wamejichimbia kwenye milima ya Tora Bora.

 

Miaka ya tisini, Urusi nayo iliyatumia mabomu haya katika vita yake na Chechnya huku Rais wa Syria, Bashar al-Assad akidaiwa kuyatumia kwenye vita dhidi ya waasi wa utawala wake.
Richard Manyota

Leave a Comment