×

Sure Boy, Bangala Wapewa Kazi Maalum Yanga

 

MARA baada ya Yanga kuwakosa wachezaji wake mahiri, Khalid Aucho na Djuma Shabani katika mchezo wao wa leo Jumapili dhidi ya Geita Gold utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amewatuliza mashabiki na kuwaambia kila kitu kitakuwa sawa.

 

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanatarajiwa kuwakosa wachezaji hao kutokana na Aucho kupata majeraha, huku Djuma akiripotiwa kuwa na malaria.

Wakati nyota hao wakikosekana, eneo la kiungo linatarajiwa kuchezwa na Yanick Bangala sambamba na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ wakisaidiana na nyota wengine akiwemo Feisal Salum ‘Fei Toto’.

 

Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold walipokutana mzunguko wa kwanza Uwanja wa Mkapa, Dar, bao la ushindi likifungwa na winga Jesus Moloko.

 

“Tutawakosa Aucho na Djuma Shabani katika mchezo dhidi ya Geita, lakini sio sababu ya kushindwa kupata matokeo mazuri, bado tuna machaguo mengine bora katika kikosi chetu ambayo yanaweza kupambana kwa ajili ya timu.

 

“Ni mchezo mgumu ambao tunahitaji kupata matokeo mazuri, wachezaji wanafahamu wanatakiwa kushinda na tunatakiwa kuwa bora sana dhidi ya wapinzani wetu ili kufikia malengo,” alisema kocha huyo raia wa Tunisia na kuongeza.

 

“Yanga kila mchezaji ambaye amesajiliwa msimu huu tumemuamini kwamba anaweza kuja kuongeza thamani kwenye kikosi, hatujasajili mchezaji wa kulipwa mshahara bila kufanya kazi, hivyo licha ya kwamba tutawakosa baadhi ya wachezaji, lakini hilo halitutishi katika mpango wa kupata alama tatu.

 

“Tuna kikosi kikubwa ambacho kinaweza kucheza katika mazingira yoyote na tukapata matokeo mazuri, kikubwa tunaamini Geita ni timu nzuri ambayo itaonesha ushindani mkubwa, lakini malengo ni kuondoka na alama tatu mbele yao”

 

GEITA WAJIBU MAPIGO

Wakati Yanga ikiingia uwanjani leo ikiwa timu pekee katika Ligi Kuu Bara msimu huu haijapoteza mechi baada ya kushuka dimbani mara 16, Geita Gold kupitia kwa kocha wake msaidizi, Mathias Wandiba ‘Master’ ameahidi kuitibua rekodi hiyo.

 

“Tumekuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi, kiukweli tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata ushindi mbele ya Yanga, shabaha yetu ni kuona tunapata matokeo chanya kwenye uwanja wa nyumbani.

 

“Tumecheza michezo nane mfululizo bila kupoteza kwenye uwanja wa nyumbani, hivyo tumejiandaa kushinda dhidi ya Yanga licha ya kwamba mpaka sasa hawajapoteza mechi, ninaamini sisi tunakwenda kuwa timu ya kwanza kupata ushindi mbele yao.”

 

WAANDISHI: JOHNSON JAMES, MARCO MZUMBE NA MUSA MATEJA

Leave a Comment