
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetembelea kiwanda cha bia cha Kampuni ya Serengeti (SBL) cha Dar es Salaam na kuelezea kuridhishwa na uwekezaji inayofanya kampuni hiyo hapa nchini.

Akiongea katika ziara hiyo iliyolenga kuangalia namna zoezi la utekelezaji wa stempu za kielekroniki unavyoendelea, mwenyekiti wa bodi hiyo, Ulledi Mussa alisema uwekezaji unafanywa na SBL una tija kubwa kwa taifa.

“Upanuzi mkubwa wa viwanda vyenu unaonyesha kuwa mpo na mtanendelea kuwepo. Serikali ipo nyuma yenu na changamoto mbalimbali za kikodi zitakuwa zikiendelea kufanyiwa kazi ili kuwawekea mazingira mazuri zaidi ya kufanya biashara zenu,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa TRA inaichukulia kampuni ya SBL kama mdau muhimu wa maendeleo na kushukuru kwa uwekezaji wake katika miradi mbalimbali ya kijamii.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa mahusiano kwa umma wa SBL John Wanyancha alisema kampuni hiyo imekuwa ikiwekeza katika miradi mbalimbali ya kijamii kama vile maji, elimu, kilimo endelevu na mingineyo.