
KAMPUNI ya runinga ya kidigitali ya Dstv ambayo imekuwa mkombozi wa wasanii wa filamu za hapa nchini maarufu Bongo Muvi imeshusha neema nyingine kwa wasanii hao kwa kufungua soko la kununua kazi zao na kuwawezesha mtaji wenye nia ya kutengeneza kazi na hawana mitaji.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu nchini, Emmanuel Ndumukwa amesema Kampuni ya Dstv kupitia chanel yao ya Maisha Magic Movies imekuja na neema nyingine kwa soko la filamu za hapa nchini kwa kununua kazi kutoka kwa waandaaji na fursa nyingine ni kutoa mitaji kwa waandaji wa filamu hizo ambao hawana mitaji.

Mkurugenzi baada ya kuzungumza hayo alimpisha Mkuu wa Chanel hiyo, Barbara Kambogi ambaye alianza kuweka bayana fursa hiyo jinsi itakavyowanufaisha waandaaji hao.
Barbara amesema wameamua kuja na fursa hiyo kwa waandaaji wa filamu wa Afrika Mashariki kutoka nchi ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Ameendelea kusema kuwa;
“Ndugu wanahabari kama mnakumbuka Julai mwaka jana tuliwatangazia kuwa tunakuja na chanel mpya ambayo italenga zaidi nchi tatu za Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya na Uganda na sasa ndiyo tumefanya kama tulivyowaahidi.

“Fursa hii itatumika kununua kazi za muvi za nchini hizo na kuzionesha kwenye chanel ya Maisha Magic Movies.
“Hivyo basi baada ya kusema hayo natangaza rasmi kuwa kuanzia sasa dirisha lipo wazi na wadau waanze kutuletea kazi zao,” alisema Barbara.
Barbara amesema kwa anayehitaji kupeleka muvi yake aingie kwenye tovuti yao ya M-Net na kuchagua tovuti ya Maisha Magic Movies na utakuta fomu ambayo utaijaza na kuambatanisha na link ya filamu yako.
Baada ya kufanya hivyo Dstv watakaa na kuijadili na ikikubaliwa basi watafanya biashara na muandaaji huyo.
Akitangaza fursa nyingine Barbara amesema wameanzisha utaratibu kuwawezesha mitaji waandaji wa filamu ambao wana mawazo ya filamu lakini hawana mitaji ambapo amesema wanawawezesha mitaji ya mpaka milioni 23 kwa filamu mmoja ambayo itakubaliwa.
“Kama wewe ni muandaaji wa filamu unachotakiwa ni kuingia kwenye tovuti yetu ya M-Net kutuwekea mswada ya hiyo filamu, majina ya utakaowashirikisha pamoja na bajeti yako ambapo tukiridhika na hiyo filamu tutakuita na kukufanyia usaili na ukipita kwenye huo usaili tunakupa hilo fungu unalohitaji.
“Hivyo tunawaomba wadau wachangamkie pia fursa hiyo ili tuiendeleze tasnia hii” alimaliza kusema Barbara.
Naye Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Eliah Mjata akizungumza baada ya kutangazwa neema hiyo ameishukuru Bodi ya Filamu kupitia Katibu wa Mtendaji Dk. Kiagho Kilonzo kwa kuendelea kuwatafutia masoko kutoka sehemu mbalimbali kila kukicha ikiwemo neema hiyo kutoka Dstv ambayo itazidi kuongeza heshima na kipato kwenye tasnia ya filamu hapa nchini.