
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia kamisheni ya utalii, imesema uchunguzi wa madai ya mtalii kutoka Nigeria, Zainab Oladehinde anayedai kwamba alidhalilishwa kingono katika Hoteli ya Warere visiwani humo, umeanza mara moja.
Taarifa iliyotolewa na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, inaeleza kwamba imepokea taarifa hizo kwa masikitiko na kwamba uchunguzi wa kina utafanyika kubaini ni nini kilichotokea na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wahusika.
Zainab ameibua madai mazito kwenye mitandao ya kijamii, akidai alinusurika kubakwa katika hoteli hiyo, baada ya mtu asiyefahamika kuingia chumbani kwake usiku na kujaribu kumuingilia kimwili bila ridhaa yake.
Uongozi wa Hoteli ya Warere, nao umejibu tuhuma hizo nzito na kueleza kwamba Zainab alikubaliana na mmoja wa walinzi wa hoteli hiyo kwamba aende chumbani kwake usiku ajili ya kukutana kimwili lakini baadaye aligeuza maneno na kudai kwamba alitaka kubakwa.
Taarifa ya hoteli hiyo, inaeleza kwamba suala hilo lilipelekwa polisi ambapo ilishauriwa lipelekwe mahakamani lakini Zainab alikataa na badala yake akataka alipwe dola 10,000 za Kimarekani kama fidia.