×

Old Trafford, Manchester United Itakuwa na Kibarua Kizito Dhidi ya Chelsea leo

KATIKA Uwanja wa Old Trafford, leo Alhamisi, Manchester United itakuwa na kibarua kizito mbele ya Chelsea ukiwa ni mchezo wa Premier League.

Man United itacheza na Chelsea ikiwa kama imepoteza matumiani ya kutinga top four, kwa sasa ina pointi zake 54, huku wapinzani wao wakiwa na pointi 65 wakishika nafasi ya tatu katika msimamo wa Premier League.

 

Kumbuka katika misimu miwili iliyopita kwenye Premier, 2019/20 na 2020/2021, timu hizo zilipokutana mara nne, Man United alishinda mbili na sare mbili.

Katika mchezo uliopita, wawili hawa walipokutana ndani ya Stamford Bridge walitoka sare ya bao 1-1.

 

Mchezo huu wa leo kila mmoja atakuwa akicheza kusaka pointi tatu kwani zina maana kubwa kwao.

Chelsea ataendelea kupambana kuona anasalia ndani ya top four, lakini Man United wao ni kuona wanamaliza nafasi za juu ili kucheza hata Europa League. Kwani vita ya top four ni kama imekolea kwa Arsenal na Tottenham.

 

Man United watakuwa nyumbani leo wakiwa na machungu ya kutoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Arsenal ugenini kwa mabao 3-1.

Leo zinakutana timu mbili ambazo moja inaonekana imara zaidi ambayo ni Chelsea, Man United wanaonekana wabovu, lakini mchezo uliopita, Chelsea pia walikuwa imara, mechi ikaisha kwa sare ya 1-1.

Katika mchezo ule, Chelsea walipiga mashuti 24 na Man United wakapiga matatu.

 

Matumaini makubwa ni kuwa katika mchezo huu huenda Man United ikawa na Cristiano Ronaldo aliyekosekana awali, kwa siku za karibuni ndiye mchezaji pekee ambaye anafunga mabao mara kwa mara.

Ronaldo huenda akafufua matumaini ya top four kwa Man United, mbele ya Chelsea ambao kwa siku za karibuni wamekuwa hawatabiriki, nyota wao wengi ni kama viwango vimeshuka tofauti na walivyoanza awali.

 

United ambao watakuwa nyumbani wanatakiwa kupambana kwa tahadhari kubwa hasa eneo la ulinzi ambalo limekuwa na makosa ya mara kwa mara.

 

Chelsea licha ya kutokuwa na kiwango cha mwendelezo, lakini nyota wake kama Christian Pulisic, Kai Havertz na Mason Mount wamekuwa tishio kwa kutupia, hivyo Harry Maguire na mabeki wenzake wanatakiwa kujipanga kweli.

Ubora wa mabeki na safu yao ya ushambuliaji ndiyo imekuwa ikiwabeba Chelsea kwa kiasi kikubwa tofauti Man United.

 

Kwa maana hiyo, hautakuwa mchezo rahisi zaidi hasa kwa United, wasipochanga karata zao vema basi mambo yataendelea kuwa mabaya upande wao washindwe hata kumaliza ndani ya top six jambo ambalo litakuwa ni la aibu kubwa kwa misimu ya karibuni.

VIKOSI

MAN UNITED: De Gea, Maguire, Varane, Telles, Dalot, Matic, McTominay, Sancho, Ronaldo, Bruno na Elanga.

CHELSEA: Mendy, Azpilicueta, Silva, Chalobah, Rudiger, Kante, Jorginho, Alonso, Mount, Werner, Havertz

MATOKEO MAN U VS CHELSEA

MECHI: 10

MABAO: 20

Chelsea             1-1 Man United

Chelsea             0-0 Man United

Man United      0-0 Chelsea

Chelsea             0-2 Man United

Man United      4-0 Chelsea

Man United      1-1 Chelsea

Chelsea             2-2 Man United

Man United      2-1 Chelsea

Chelsea             1-0 Man United

Man United      2-0 Chelsea

Leave a Comment