×

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO) – 14

 

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

“Unamuona legelege huyu! Ohoo, muangalie hivyohivyo,” alisema Bonta ambaye alikuwa akizunguka huku na kule akiendelea na kazi ya kukagua kama kazi zilikuwa zikifanyika vizuri.

 

“Msimulie hiyo alama hapo usoni umeipataje,” alisema Bonta huku akicheka, nikajikuta nikitabasamu kwa sababu kauli yake hiyo ilinikumbusha kuhusu lile tukio la yule kondakta mpuuzi aliyetaka kunieletea ubabe na mwisho akaishia kutimua mbio kama mtoto mdogo.

 

SASA ENDELEA…

“Eti umefanya nini kwani?” Mzee Shekwavi alizidi kunidadisi lakini sikuwa tayari kumweleza chochote, hakuna kitu nilichokuwa sikipendi kama kudharauliwa. Basi alipoona nimekasirika, hakutaka kuendelea kunihoji, akaanza kunipangia majukumu ya kazi.

 

Aliniambia kwa siku hizo za mwanzo, kazi yangu itakuwa ni kuosha magari, nje na ndani huku pia nikisaidia kazi nyingine nitakazokuwa natumwa. Nilikubali na bila kupoteza muda, alinionesha gari dogo lililokuwa pembeni kidogo, akaniambia natakiwa kuanza na gari hilo.

 

Ainielekeza na vifaa vyote vinavyohusika, ikiwemo mpira maalum wa maji ambao unaunganishwa kwenye bomba na kuongeza presha ya maji, sabuni, dawa maalum za kutoa madoa na vifaa vya kukaushia ndani ya gari.

 

Binafsi niliiona kama ni kazi nyepesi ambayo haiwezi kunishinda chochote na moyoni nikajiapiza kujifanya kwa moyo wangu wote na kwa nguvu zangu zote. Nilianza kuliosha gari hilo upande wa nje na nilijitahidi sana kuling’arisha, lakini nikagundua kwamba kuna kioo kimoja kilikuwa kimetoka.

 

Basi sikujali sana, nilipomaliza kulisafisha kwa nje, nilihamia kwa ndani na hapo ndipo nilipogundua vitu vilivyonishtua sana moyo wangu. Kwanza niligundua kwamba kile kioo kilichopasuka, kumbe ni kile kilichopo upande wa dereva kwenye mlango wa mbele, lakini pia upande wa ndani, siti yote ilikuwa imelowa damu ambazo sasa zilikuwa zimekauka huku zikiwa zimechanganyikana na vioo ‘vilivyomwagikia’ kwa ndani.

 

Yaani kwa mazingira yale, ilitosha kabisa kuelewa kwamba kulikuwa na tukio baya lililohusisha gari hilo. Ilibidi nijikaze kiume na kuendelea na kazi kwani kuna wakati nilimuona mzee Shekwavi akinitazama kwa macho ya kuibia.

 

Nadhani alikuwa anajua kila kitu lakini akataka kuona nitachukua uamuzi gani. Japokuwa nilikuwa nimeshtushwa sana ndani ya moyo wangu, lakini nilijikaza kisabuni, nikaanza kusafisha palepale kwenye ile siti, nikakusanya na kutoa vipande vyote vya vioo, nikachukua ile dawa maalum ya kutoa madoa na kuimwagia kwenye siti yote, nikachukua brasi kubwa na bomba la maji.

 

Nilianza kusafisha damu zile ambazo nilikuwa najua kabisa kwamba ni za mtu, nikaendelea kupiga brashi kwa nguvu huku nikijifanya kama hakuna chochote kilichotokea. Nilipomaliza, niliendelea na siti ya pembeni yake, napo nikapasafisha, nikahamia siti za nyuma na kuzisafisha na baada ya muda, nilikuwa nimemaliza ingawa pale kwenye siti ya dereva bado kulikuwa na madoa ya damu kwa mbali.

 

Kumbe hakuwa Shekwavi pekee aliyekuwa akinitazama, ilionesha ni kama gari hilo lilikuwa limewekwa kama kipimo maalum kwa ajili yangu, kwani kumbe Bonta naye alikuwa amekaa sehemu an kujificha akifuatilia kila kilichokuwa kinaendelea na hata wale waliokuwa wakijifanya wanafanya mazoezi, nao walikuwa wakinifuatilia bila mwenyewe kujua.

 

Nilipomaliza ndipo nilipogundua kwamba kumbe nilikuwa nafuatiliwa, moyoni nikawa najiuliza sasa walitegemea nitakimbia baada ya kuona damu za mtu? Au walitegemea nitapiga kelele?

 

Nisingeweza kufanya hivyo kwa sababu kuanzia mazingira niliyochukuliwa na kina Bonta na wenzake mpaka muda huo, tayari ndani ya kichwa changu nilishaelewa wao ni watu wa aina gani na nimeingia kwenye kundi la aina gani na sikuona kama kuna tatizo lolote kwa sababu nilikuwa nahitaji fedha, kichwani sina elimu wala sina mtu yeyote ninayefahamiana naye.

 

Naomba ieleweke kwamba tayari nilishajua kwamba kundi lile linahusika na nini lakini niliamini kazi zangu mimi zitakuwa ni hizo ndogondogo tu, labda za kutumwa kununua vifaa, kusafisha magari, kuhesabu fedha na nyingine za namna hiyo.

 

Sikuwahi kudhani kwamba kwa kukubali moja, maana yake nimekubali mbili na tatu! Sikufikiria kwamba Bosi Mute ambaye katika hatua hizo za awali alikuwa mtu muhimu sana kwangu, anaweza kuniingiza kwenye kazi ya hatari kama kushika mtutu wa bunduki, tena nikiwa na umri mdogo kiasi hicho na ndiyo maana hata baadaye alipokuja kunigeuka, ugomvi kati yetu ulikuwa mkubwa mno.

 

Basi kwa kifupi ni kwamba niliendelea kufanya kazi hiyo ya kusafisha magari ambayo ilionesha yamepatikana kwa njia za kumwaga damu kwani kila nililokuwa nasafisha, ndani ilikuwa ni lazima nikute damu, maganda ya risasi, madawa ya kulevya na kadhalika.

 

Mimi kazi yangu ikawa ni kuyasafisha na kuondoa ushahidi wote, kisha baada ya hapo yanaingizwa gereji ambapo yalikuwa yakifumuliwa na kubadilishwa kila kitu. Yaani gari likitoka, unasema ni jipya kabisa kwani linakuwa limebadilishwa kila kitu.

 

Nakumbuka siku moja, majira ya mchana nikiwa naendelea na kazi, kuna gari moja liliingizwa kwa kasi kubwa na akina Bonta na kuletwa pale ‘parking’, nikaambiwa natakiwa kulishughulikia kama kawaida lakini tofauti na magari mengine yote, hili lilikuwa na jambo la tofauti ambalo nikiri wazi kwamba ulikuwa ni mtihani mkubwa kwangu.

 

Ndani ya gari hilo, kulikuwa na mwili wa mwanamke aliyekuwa amepigwa risasi kichwani na kufa papo hapo, lakini siti ya nyuma kulikuwa na mtoto mdogo aliyekuwa amekaa kwenye vile viti maalum vya watoto vinavyofungwa juu ya siti ili kuzuia mtoto asianguke.

 

Nilishtuka kupita kawaida, niligeuka na kutazama huku na kule, kama kawaida, kila mtu alijifanya yuko bize na kazi zake lakini niligundua kwamba karibu wote walikuwa wakinifuatilia kwa makini nitakachokifanya.

 

Nilifunga mlango haraka, nikanyanyua vifaa vyangu vya kazi na kugeuka huku na kule tena, bado watu walikuwa wakinitazama kwa macho ya chinichini. Kwa kuwa pale mwenyeji wangu alikuwa ni Bonta, ilibidi niweke vifaa vyangu vya usafi na kumfuata.

 

Alikuwa amekaa kule kwenye vifaa vya mazoezi na mkononi alikuwa na chupa ndogo ya pombe kali huku pia akivuta ‘sigara’. Nilimsogelea mpaka pale alipokuwa amekaa lakini nikagundua kwamba hakuwa akivuta sigara kama nilivyodhani kwa mbali.

 

Alikuwa akivuta bangi na japokuwa sikuwa nimewahi kuvuta, nilikuwa naijua harufu yake vizuri.

 

“Braza,” nilimuita huku nikiwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu. Akanionesha kwa ishara kwamba nikae, kweli nikakaa kwenye vile vyuma vya mazoezi huku nikipumua kwa nguvu. Nilishapaniki! Sikia tu hivihivi lakini usiombe kushuhudia aliyefariki kwa kupigwa risasi.

 

“Huu ni mtihani wa mwisho kwako, bosi anataka kukupima kama una moyo wa kiume,” aliniambia kwa sauti ya chini huku akiendelea kuvuta moshi mwingi na kuumeza kisha kushushia kwa ile pombe iliyoonesha ni kali kwelikweli maana alikuwa akikunja uso anapomeza.

 

“Pale pembeni ya pipa la taka, kuna mfuko mkubwa, unatakiwa kwenda kuuchukua, utaweka ndani kile ulichokiona kwenye siti ya mbele kisha utaweka juu ya lile toroli. Maelekezo mengine utapewa,” alisema Bonta huku akiwa ‘siriasi’ sana.

 

Sikuwahi kumuona akiwa kwenye sura kama hiyo, nilishindwa hata nimjibu nini kwani nilihisi mate yakinikauka mdomoni, akanionesha kwa ishara kwamba niiunuke na kuondoka.

 

Kiukweli kama nisingewahi kushikilia bomba la moja kati ya vifaa vya kufanyia mazoezi, pengine ningeanguka mzima-mzima kwani miguu ilikosa nguvu kabisa, nikawa natetemeka mwili mzima huku miguu ikigongana.

 

Bonta alinitazama bila kusema chochote, akawa anaendelea kuvuta mibange kwa fujo, nikashusha pumzi ndefu na kusimama vizuri kwa sekunde chache. Sikuwa na uwezo wa kukataa kazi ile ngumu na ya kutisha mno.

 

Nilipiga moyo konde na kushusha pumzi ndefu kwa mara nyingine, nikaanza kutembea kuelekea kule kwenye pipa la takataka.

 

Bado nilikuwa najua kwamba watu wote wananitazama na sijui ni nini kilinitokea, lakini nilijikuta nikipata ujasiri wa kuwaonesha waliokuwa wakinitazama kwa macho ya chinichini kwamba na mimi ni mwanaume shupavu.

 

Nilienda mpaka pale, kweli nikakuta kuna mfuko mkubwa ambao upo katika mfumo wa kama nailoni ngumu, wenye zipu. Nikauchukua na kuelekea kwenye lile gari. Ambacho sikuweza kukizuia ni mapigo yangu ya moyo kwenda mbio.

 

Basi nilipofika, niliubwaga ule mfuko chini, nikachukua tena vile vifaa vyangu vya kuoshea magari, ikabidi niendelee kujifanya kama naoshaosha lile gari kwa nje. Ilikuwa ni kama kuzuga tu ili nipate ujasiri wa kufanya ile kazi ambayo ama kwa hakika ilikuwa ni mtihani mkubwa mno katika maisha yangu.

 

Sikutegemea kama naweza kukutana na kitu kama hicho maishani mwangu, kichwani maneno ya mama alipokuwa ananikataza kuja mjini yakawa yanajirudia lakini nilipokumbuka kwamba ni usiku uliopita tu nimetoka kuwaachia kiwango kikubwa cha fedha nyumbani kwa ajili ya matibabu ya baba, nilijikuta nikijiambia ndani ya moyo wangu ‘potelea mbali’.

 

Nilichukua mfuko na kuuweka vizuri, nikafungua zipu na kuingia nao ndani ya lile gari ambalo lilikuwa likinuka damu, tena damu mbichi. Nilishindwa kumtazama yule mtu kwa jinsi alivyokuwa amefumuliwa kichwa kwa risasi, nikamvalisha ule mfuko huku nikiwa makini nisichafue nguo zangu na damu.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave a Comment