
USIKU wa kuamkia leo mashabiki wa muziki wa dansi walifurika Viwanja vya Gwambina Lounge zamani TCC Chang’ombe, Dar kushuhudia mpambano wa bendi tano zilizokuwa zikifanya tamasha la pamoja ambapo Mkurugenzi wa Kampuni ya Mo Green International Limited, Patrick Kessy ambaye ndiye mdhamini mkuu wa tamasha hilo naye alionesha umahiri mkubwa baada ya kuvamia jukwaa na kuonesha kipaji chake katika muziki.

Bendi hizo ni Mjengoni Classic kutoka Arusha, Bogoss Musica, Msondo Music, Mapacha Music za Dar pamoja na Waluguru Orijino kutoka mkoani Morogoro Mji Kasoro Bahari.
Onesho hilo lilitawaliwa na burudani kibao ikiwemo wanamuziki na wanenguaji wa bendi zote kila mmoja kuonesha umahiri na kutaka kuonekana kumfunika mwenzake.

Miongoni mwa burudani zilizonogesha tamasha hilo ni makamuzi aliyofanya Mkurugenzi wa Kampuni ya Pembejeo za Kilimo na Wasambazaji wa Viuatilifu ya Mo Green International Limited, Patrick Kessy ambaye ni mdhamini wa tamasha hilo.
Mambo yakiwa yamenoga Patrick Kessy alivamia jukwaa huku akisindikizwa na Bendi ya Waluguru Orijino ambapo alifanya makamuzi yaliyowaacha hoi mashabiki waliofurika kwenye tamasha hilo ambao walilipuka kwa mayowe ya kumshangilia.

Viwanjani hapo umati mkubwa ulifurika huku suala kubwa likiwa ni kuserebuka kula na kunywa hali iliyoonekana kama vile enzi za burudani ya muziki wa dansi kurudi kwa kishindo.
HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL