
KAJALA Masanja au Mama Pau; ni staa mkubwa wa filamu nchini Tanzania mwenye umri wa miaka 40 (amezaliwa Julai 22, 1980) ambaye hatimaye amekubali msamaha wa Harmonize na hata kurudiana naye tayari kulingana na matukio ya hivi karibuni.
Mama Pau hatimaye amejibu posti moja ya Harmonize kwenye Instagram kwa mara ya kwanza tangu walipokosana zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Harmonize au Konde Boy Mjeshi ameposti ujumbe mrefu a.k.a gazeti akimshukuru Kajala kwa kusimama naye katika hali zote licha ya mabaya aliyomtendea.
“Wakati Dunia nzima inasema haiwezekani ulisimama ukasema inawezekana. Ulinipenda nami mbaya zaidi ulikutana na disappointment ambayo iliwapa nguvu na ujasiri kila mtu aliye karibu yako kusema mimi sio binadamu wa kuwa hata karibu yako. Najua uliumia sana…!!!!
“Bado hukunikatia tamaa. Wakati mwingine binadamu huingia kwenye mahusiano ukiamini kwamba unaweza kumsahau yule uliyekuwa naye mwanzo bila kuwaza nini kiliwafanya muwe pamoja.
Nilipitia hicho kipindi na picha zikamwagika mtandaoni na nikajiona nimemaliza wala sikujali maumivu yako.
“Bado ulikaa kimya, hakuna mahojiano licha ya kuahidiwa marundo ya pesa ambayo ungeweza kununua hata hivyo vigari wanavyoviona ni kitu cha maana sana,” Harmonize ameandika chini ya picha ya Kajala.
Harmonize anaendelea kufunguka kuwa tayari anayajuta mabaya yote ambayo alimtendea Kajala pamoja na familia yake.
Anasema tattoo ya Kajala na binti yake, Paula ambayo amechora kwenye mguu wake ni ishara ya majuto na ombi la msamaha kwake litakalosalia pale daima.

“Hakuna ambacho kitabadilisha kuwa nilikosea familia yangu. Hakuna ambacho kitabadilisha kuwa ni familia yangu. Pia hakuna ambacho kitabadilisha kuwa najivunia familia yangu mguu wangu wa kulia utasema sorry mpaka siku yangu ya mwisho,” anasisitiza Konde Boy.
Harmonize anasema anaumizwa sana na kejeli ambazo amekuwa akipokea kutokana na juhudi zake za kuomba msamaha.
Anaahidi kuwa anajaribu kuwa mume bora kwa Kajala.
“Nakupenda sana mke wangu Frida Kajala,” anasema Teacher Konde.
Ni wazi kuwa ujumbe huo mrefu umemfikia mlengwa kwani chini yake, Kajala amejibu kwa emoji za makopakopa zinazoashiria pongezi na upendo kwake.
Jibu la Kajala limewasisimua mashabiki wengi wa Harmonize ambao wamejumuika na kuacha jumbe nzuri za kuwatakia kila la kheri.
Cc; @sifaelpaul