
WAZIRI MKUU wa Uingereza Boris Johnson ameshinda matokeo ya kura ya kutokuwa na imani naye baada ya kupata kura 211 dhidi ya kura 148 ambazo hazikuwa na imani naye.
Hali hiyo imekuja baada ya wabunge wa chama chake cha Conservative kupiga kura usiku wa kuamkia leo juu ya kutokuwa na imani naye.
Uongozi wake umekuwa ukichunguzwa kufuatia kashfa ya uvunjwaji Sheria ndani ya Ofisi yake wa COVID-19 Mwaka 2020 na 2021.

Kwa mujibu wa sheria ya Uingereza, akishinda kura ya kutokuwa na imani naye, haiwezekani tena kumpigia kura ya namna hiyo mpaka mwaka mzima upite.
Ikumbukwe kuwa, Theresa May alishinda kura ya kutokuwa na Imani naye mnamo Januari 16, 2018 kwa kura 325 kwa 306 lakini miezi minne baadae alijiuzulu ndipo akaingia Boris Johnson.
Tony Blair naye alikumbana na vigingi mpaka akajiuzulu Mei 10, mwaka 2007, David Cameron naye ni hivyo hivyo alijiuzulu Juni 24, 2016. Je, Boris Johnson atatoboa?