
WASANII wa kike wa Bongo Muvi wanaounda kundi la Binti Filamu Foundation sasa wameamua kuja na kongamano la dawa za kulevya litakalofanyika Makumbusho ya Taifa Posta jijini Dar, Julai 1 mwaka huu.
Akizungum za na mwandishi wetu Mwenyekiti wa Binti Filamu Foundation, Ndumbagwe Misayo maarufu Thea amesema wameamua kuja na kongamano hilo ili kuliokoa taifa letu kutokana na janga la dawa za kulevya ambalo ni chanzo cha ngono zembe ambapo ndiyo chanzo cha maambukizi ya ukimwi afya ya akili, amesema Thea.

Msanii huyo aliendelea kusema;
“Sisi kama wasanii wa kike tunaounda Binti Filamu Foundation tumeamua kuja na dhana hii lengo letu kuu likiwa ni kumkomboa mwanamke kwakuwa mwanamke akishaathirika na dawa za kulevya madhara yake ni makubwa zaidi.
Unajua mwanamke anapoathirika na dawa za kulevya inakuwa pigo kwa mama mwenyewe, baba na watoto na mbaya zaidi kama mama ni mjamzito huku akitumia dawa za kulevya zinamuathiri mtoto tumboni moja kwa moja.

Ndiyo maana tumeona kama wasanii wa kike tuje na mpango huu ili kumkomboa mwanamke na wengineo hivyo tunawaomba wamama, wadada wakaka na wababa wote mje kwa wingi kwenye kongamano hilo litakaloanza saa tatu asubuhi mpaka saa saba mchana ambalo halina kiingilio.
Thea alisema katika kongamano hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Dorothy Gwajima. Katika mkutano huyo Thea aliambatana na wasanii wenzake wa Binti Foundation, Blandina Chagula ‘Johari’, Mayasa Mrisho ‘Maya’ Joan Mutovolwa na wengineo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa filamu nchini, Emmanuel Ndumukwa aliyemuwakilisha Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt. Kiagho Kilonzo amesema wao kama serikali wanawaunga mkono Binti Filamu Foundation kwa mpango huo waliokuja nao ambao una lengo la kukiokoa kizazi kilichopo na kijacho.
Mkurugenzi Ndumukwa aliendelea kusema;
“Sisi kama serikali tunawaunga mkono moja kwa moja wasanii hawa kwa mpango wao huu wenye lengo la kukiokoa kizazi kilichopo na kijacho. Dawa za kulevya zimeshawaathiri wengi sana wakiwemo wasanii wa fani mbalimbali ambao wengine mpaka muda huu wako kwenye vituo vya ‘soba’ kwa ajili ya kurekebisha mwenendo huo mbaya na kwingineko.
“Hivyo tunawaomba wananchi wote na wadau mbalimbali tujitokeze kwa wingi kwenye kongamano hilo ambapo watakuwepo wadau mbalimbali wakiwemo watu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya na washauri wengine”. Alimaliza kusema Mkurugenzi Ndumukwa.
HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL