×

Rais Samia Atoa Rai kwa Viongozi wa Dini Kuelimisha Waumini Juu ya Utunzaji wa Mazingira

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongea katika maadhimisho ya mkutano wa 20 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaasa viongozi wa Dini kuendelea kuwaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kwa ajili ya maendeleo ya kizazi kilichopo na kijacho.

 

Rais Samia ameyasema hayo katika maadhimisho ya mkutano wa 20 wa AMECEA ambayo ni Jumuiya ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki ambapo amesisitiza juu ya vita ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi huku akibainisha kuwa vita hiyo si ya mtu mmoja bali ni ya watanzania wote.

Maaskofu Katoliki wakisikiliza Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais Samia amenukuliwa akisema:

“Vita hii si ya mmoja kwani mazingira yakichafuka, ni majanga kwa kila viumbe vyote na ulimwengu mzima kwa ujumla.”

 

Rais Samia amesema inatia moyo kuona Baba Mtakatifu wa kanisa Katoliki Duniani Papa Francis kuona suala la utunzaji wa mazingira linakuwa sehemu ya ujumbe na mpango mkakati kwa Maaskofu na waumini wa dini ya Kikristo kote Duniani.

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki nchini Kardinali Polycarp Pengo

Aidha Rais Samia amesema Tanzania inathamini maisha ya kijamii yanayoendana na mantiki ya mkakati wa utunzaji wa mazingira ambao pia umechagizwa na Kanisa Katoliki.

Leave a Comment