
Wananchi Mkoani Mbeya wanatarajia kunufaika na kiasi cha shilingi bilioni 18.2, pesa zilizotengwa kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.
Mhandisi Florian Kabaka,ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), amebainisha hayo wakati wa ukaguzi wa Daraja la Mwasanga linalounganisha kata za Mwakibete na Tembela, Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Alieleza kuwa pamoja na ujenzi wa Daraja la Mwasanga litakalogharimu kiasi cha shilingi 1,985,044,200, fedha hizo zitajenga kwa kiwango cha lami barabara za Inyala-Simambwe (km 16.7) shilingi 7,052,878,707; Lupeta-Izumbwe (km 10) shilingi 4,516,401,000; Masebe-Lutete(km 7.2) shilingi 2,577,042,388; na Masebe-Bugoba kibaoni (km 5) shilingi 2,123,900,000.
Aidha mhandisi Kabaka aliagiza watendaji kuongeza usimamizi na kulipa wakandarasi kwa wakati ili kusiwe na kisingizio chochote, kwa kuwa fedha zipo.
Kwa upande mwingine ndugu Maonyeshwe Mbwiga mkazi wa Mwakibete aliishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja litakalo waondolea kero walizokuwa wakipata.

Naye Aron Nyembele, mwanafunzi wa Sekondari Mwakibete alisema kuwa walikuwa wanapata shida kuvuka baada ya daraja kubomoka na wamefurahi kuona daraja jipya na la kisasa linajengwa.
Bodi ya Ushauri TARURA inaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mbeya kukagua miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na iliyo kamilika ili kuhakikisha adhma ya Serikali ya kuboresha na kufungua barabara mpya za Vijijini na Mijini na kuwaletea maendeleo wananchi inatimia.