
MSHAMBULIAJI wa Klabu ya Borussia Dortmund raia wa Ivory Coast Sebastien Haller amegundulika kuwa na matatizo ya saratani ya tezi dume ikiwa ni muda mchache baada ya kufanya mazoezi na klabu yake mpya aliyohamia akitokea klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi.
Haller amesajili wa Dortmund akitokea Ajax kwa ada ya Euro milioni 31 kwa ajili ya kuziba pengo la Erling Haaland aliyetimkia katika klabu ya Manchester City ya nchini Uingereza.

“Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Sebastien Haller amegundulika kuwa na matatizo ya Saratani ya tezi dume na ameruhusiwa kuondoka katika kambi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya iliyopo Bad Ragaz nchini Switzerland na kurejea nchini Ujerumani kwa ajili ya vipimo zaidi.” Imesema ripoti ya klabu hiyo.

Haller (28) amemaliza msimu uliopita ikiwa ni moja ya misimu yake bora katrika maisha yake ya soka akifanikiwa kufunga jumla ya mabao 34 katika mashindano yote.
Alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 11 katika hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kabla ya klabu yake kuondolewa katika hatua ya 16 bora.