
RAIS wa China Xi Jinping amemuonya Rais mwenzie wa Marekani Joe Biden achukue tahadhari kuhusu kuchezea moto kwa kujiingiza katika sakata la China na Taiwan.
Hiyo ni kufuatia mazungumzo ya tano kwa njia ya simu yaliyofanyika katika muda ambao Mataifa mengi duniani yanapambana na matatizo ya kiuchumi pamoja na utawala wa mipaka.
Chombo cha habari cha Serikali ya China kimeripoti kuwa Rais Xi alimuambia Rais Biden kuwa Marekani inatakiwa ikubaliane na sheria moja tu ya nchi ya China na kusisitiza kuwa China imesimamia msimamo wa kutotambua uhuru wa Taiwan pamoja na kutoingiliwa na mataifa ya nje.

“Wale wote wanaocheza na moto wataishia kuungua tu.” alinukuliwa Xi akimuambia Biden. Tunategemea Marekani wataliona jambo hili vizuri sana.
Taarifa kutoka White House imebainisha ya kwamba Rais Biden alimuambia Rais Xi kuwa msimamo wa sera za Marekani uko palepale na haujabadilika ambapo Washington inapinga jitihada za baadhi ya mataifa kupinga uhuru wa Taifa jingine pamoja na kuhatarisha amani na utulivu duniani.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Taiwan amemshukuru Rais Biden kwa jitihada zake na msaada anaoutoa kwa nchi hiyo nakusisitiza kuwa wataendelea kujidhatiti na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi hiyo pamoja na kuimarisha mahusiano mazuri na nchi ya Marekani.
Mazungumzo kati ya Xi na Biden yamekuja wakati ambao Marekani inatafuta njia mbalimbali ya namna ya kufanya mahusiano ya kibiashara na China kutokana na kuteteleka kwa uchumi Duniani ingawa kumekuwa na kutofautiana kwa mataifa hayo katika masula mazima ya Haki za Binadamu, Afya pamoja na Sera za Kiuchumi.