
KLABU ya Chelsea inajiandaa kuachana na nyota wake wawili ambao wanatarajia kuondoka klabuni hapo kwa mkopo wa msimu mzima.
Golikipa namba mbili wa klabu hiyo raia wa Hispania Kepa Arizzabalaga pamoja na mlinzi kinda Malang Sarr wote wanatarajiwa kuondoka klabuni hapo kwa mkopo ambapo Kepa anatarajiwa kujiunga na Napoli kwa msimu mzima huku Malang Sarr akitarajiwa kutimkia nchini Ufaransa katika klabu moja ya ligi kuu nchini humo.

Kocha mkuu wa Klabu hiyo Mjerumani Thomas Tuchel ameelekeza nguvu zake katika kukiimarisha kikosi chake ambapo klabu hiyo inadaiwa kuwa njiani kukamilisha dili la kumsajili beki wa kushoto wa klabu ya Brighton and Hove Albion Marc Cucurella anayewaniwa pia na klabu ya Manchester City.

Chelsea ambayo hadi sasa imefanikiwa kukamilisha usajili wa wachezaji wawili Raheem Sterling kutoka Manchester City pamoja na Kalidou Koulibaly bado ipo sokoni ambapo kocha wake Thomas Tuchel amebainisha kuwa anahitaji wachezaji wengine zaidi ili kuwa katika nafasi nzuri kwa ajili ya mapambano ya msimu mpya wa 2022/2023.