×

Siyo kinyozi tena, siku hizi ni saluni!

Hapo zamani za kale wakati wa enzi zetu, mkaka alikuwa akitaka kunyoa nywele anaenda kwa kinyozi na kinyozi alikuwa mwanaume. Mdada akitaka kunyoa nywele zake anamtafuta mdada mwenzie amnyoe nywele.

Vinyozi walikuwa wa aina kuu mbili walikuweko wale vinyozi ambao shughuli zao walizifanyia chini ya mti, na wengine ndiyo walikuwa wanakuwa na chumba ambacho nje utakuta kibao kimeandikwa kinyozi.

Kwa kinyozi ndiko kulikokuwa sehemu ya kupata habari mbalimbali za nini kinaendelea katika jamii. Pale kwa kinyozi wa chini ya mti watu walikuwa wakikusanyika na kila mtu kuleta hadithi zake, pembeni pia ungekuta muuza kahawa naye alikuwa akifanya biashara yake, kwa kinyozi kulikuwa kijiwe muhimu.

Wale vinyozi walianza kuwa na vyumba vya kunyolea, siku hizi mnaita fremu, wao nao walikuwa mabingwa wa stori za mjini, unaponyolewa unahadithiwa kila linaloendelea mjini. Kitu kimoja muhimu ambacho ungekikuta enzi hizo kwa kinyozi ni bango la bei.

Pale ungekuta maelezo rahisi ya bei za kunyoa. Ndevu 40/-, Kipara 20/-, denge 50/-, fashen 100/- pia ungekuta staili nyingine kama Afro, Kambona na kadhalika na bei zilikuwa wazi kabisa. Kwa hiyo ukiingia kwa kinyozi unajua kabisa utadaiwa nini.

Katika enzi hizi za kizazi cha dot.com ishu ya kunyoa imekuwa ngumu na inahitaji elimu kidogo au la utaishia polisi. Hivyo naomba nitoe darasa kwa wale jamaa zangu wa enzi za Azimio la Arusha. Kwanza siku hizi huendi kwa kinyozi unaenda saluni, saluni hukuti mzee hata mmoja wote ni vijana tena mchanganyiko wa kike na wa kiume.

Wote wamevaa nadhifu Kibongo Fleva. Saluni zina makochi, TV, feni, vimbwanga kibao. Ukifika swali litakuwa unataka nini, ukisema kunyoa ni vizuri ungetoa maelezo ya ziada, kwenye saluni hizi kuna staili moja kuu ya kunyoa nayo ni kupunyua nywele mpaka unakuwa kama vile umemaliza kifungo jana yake.

Hivyo jieleze vizuri unataka urefu gani wa nywele zibaki, japo mara nyingi hayo maelezo hakuna anayejali watakupunyua tu. Wakati uko kwenye kiti unamsubiri kinyozi aanze kazi, atakuja binti mmoja mzuri na akiwa na tabasamu la nguvu atakuuliza, ‘Mzee tukuoshe na uso?’ au ‘Mzee tukufanyie masaji ya uso?’ ushauri wangu ni kuwa kataa.
Kama ukikubali utaingizwa kachumba pembeni na kuoshwa uso na maji safi ya uvuguvugu, wakati huohuo utaulizwa tutumie lotion ya Tanzania au Kenya? Chondechonde kataa, kama utakubali utapakwa loshen safi, kisha utaambiwa pumzika feni ikupulize losheni ikolee. Wakati huo unaweza kuulizwa kama uoshwe miguu?
Ukikubali usinilaumu. Sasa pale unapoaga na kutoa alfu tatu za kunyolewa ndipo utashangaa. Unapewa bili ya kunyoa, masaji ya uso, kuoshwa uso, kupakwa losheni na kuoshwa miguu jumla alfu 70 na wewe mfukoni una alfu tatu.

Leave a Comment