
WANANCHI Yanga SC wanatamba huko mtaani wakiwaambia Simba SC: “Semeni tena.” Hiyo ni baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Msimu uliopita katika mchezo kama huo ambao Yanga walishinda 1-0, Simba walisema Yanga wamebahatisha, lakini baada ya jana kulala tena, Yanga wameamka kifua mbele na kuwaambia: “Haya semeni tena, hatujamaliza, tunabeba yote msimu huu kama msimu uliopita.”

Ni yuleyule Fiston Mayele ambaye alifunga bao pekee msimu uliopita, ndiye aliyefunga mabao mawili kwa Yanga jana dakika ya 49 na 80. Kabla ya hapo, Pape Ousmane Sakho aliifungia Simba dakika ya 16.
Mayele alipachika bao la kwanza kipindi cha pili akimalizia pasi ya Stephane Aziz Ki ambaye katika mchezo huo, aliwafanya vibaya walinzi wa Simba na kuonekana ni mtu hatari zaidi.

Makosa ya safu ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na mabeki wa kati Henock Inonga na Mohamed Ouattara, ilimpa nafasi nyingine Mayele kufunga bao la pili akiwazidi ujanja.
Licha ya mabadiliko ya wachezaji kwa upande wa Simba ambapo alitoka Chama na nafasi yake kuchukuliwa na Augustine Okrah, Sadio Kanoute nafasi yake kuchukuliwa na Mzamiru Yassin pamoja na Kyombo nafasi yake kuchukuliwa na Dejan, huku Bocco akiingia kuchukua nafasi ya Jonas Mkude, bado Simba haikuweza kupata bao lingine.
Mayele ambaye aliwavuruga vibaya walinzi wa Simba, hakuyeyusha dakika 90, alitolewa nafasi yake ikachukuliwa na Heritier Makambo, huku nahodha Mwamnyeto akiingia kuchukua nafasi ya Aziz Ki.

Yanga walionekana kuutawala zaidi mchezo huo ambapo wachezaji wake walikuwa na kasi kila wanaposhika mpira tofauti na ilivyokuwa kwa Simba.
Kumalizika kwa mchezo huo, kunamaanisha kwamba msimu wa soka hapa nchini 2022/23 umefunguliwa rasmi ambapo kesho Jumatatu, Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza.
Kikosi cha Yanga kilichoanza; Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Dickson Job, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Salum Aboubakar, Feisal Salum, Fiston Mayele, Stephane Aziz Kin a Farid Mussa.
Upande wa Simba walianza hivi; Beno Kakolanya, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Mohamed Ouattara, Jonas Mkude, Pape Sakho, Sadio Kanoute, Habib Kyombo, Clatous Chama na Kibu Denis.
STORI NA JOEL THOMAS