Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall.
Sweetbert Lukonge, Zanzibar
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amemshangaa mshambuliaji wa TP Mazembe ya DR Congo, Mtanzania, Mbwana Samatta, kwa uamuzi wake wa kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji.
Samatta ambaye ni mfungaji bora wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, yupo mbioni kutua katika Klabu ya Genk ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji, licha ya hivi karibuni TP Mazembe kudaiwa kuwa imempatia timu nyingine kutoka nchini humo ambayo pia inahitaji huduma yake.
Akizungumza na Championi Jumatano, Hall alisema kuwa kwa uwezo alionao Samatta hakustahili kabisa kucheza Ligi Kuu ya Ubelgiji ambayo ni ya kiwango cha chini kabisa barani Ulaya.
Alisema kwa uwezo wake huo alistahili kupata timu England hata kama siyo Manchester United, basi hata inayoshika nafasi ya chini kwenye msimamo wa ligi kuu ya nchi hiyo.
“Kwa uwezo wa Samatta, hakustahili kabisa kucheza soka nchini Ubelgiji kwani ligi yake ni ya chini kuliko ile ya Daraja la Kwanza ya England.
“Kama alishindwa kupata timu kutoka nchi zenye ligi bora basi ni bora angetafuta timu ya Daraja la Kwanza ya England, ambako angepambana na mwisho wa siku mambo yangekuwa mazuri kwake,” alisema Hall.
Katika hatua nyingine, Hall amewataka mawakala wanaowatafutia timu wachezaji barani Ulaya kutoridhika mapema na badala yake wanatakiwa kuhakikisha wanapambana vilivyo ili wateja wao waweze kupata nafasi kwenye ligi bora.