
SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inakaribisha wazabuni katika ujenzi wa reli ya kisasa, Standard Gauge Railway (SGR) njia ya Uvinza nchini Tanzania mpaka Gitega nchini Burundi yenye urefu wa kilomita 367 itakayopanua Reli ya Standard Gauge hadi Burundi.
Katika taarifa hiyo, wahusika wana hadi Novemba 15 kutuma zabuni zao kwa Shirika la Reli la Tanzania(TRC), kwa ajili ya kubuni na kujenga njia kutoka Uvinza magharibi mwa Tanzania hadi mji mkuu wa Burundi wa Gitega.

TRC ilisema tayari fedha zimetengwa na serikali zote mbili kwa ajili ya mradi huo kuanza ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023. Mradi huo utahusisha kilomita 282 za njia kuu na kilomita 85 za ‘loops’ za kupita. Sehemu ya kwanza itachukua kilomita 180 kutoka Uvinza hadi Malagarasi ndani ya Tanzania, na sehemu ya pili itachukua kilomita 187 kuvuka mpaka hadi Musongati na kisha Gitega.
Mradi huo umeanza kutekelezwa tangu Januari, wakati nchi hizo mbili zilipotia saini mkataba wa maelewano kuhusu makadirio ya gharama ya awali ya dola milioni 900 za kimarekani.
Imeandikwa: John Mbwambo kwa msaada wa mitandao.