
ZAIDI ya watu 10 wamefariki dunia na wengine wamenusurika kifo na kulazwa hospitalini nchini Uganda, baada ya kunywa pombe aina ya City 5 Pineapple Flavored Gin inayodaiwa kuwa na sumu.
Taarifa hiyo imetolewa na Jeshi la Polisi nchini Uganda na kueleza kuwa Polisi wa Kaskazini Magharibi mwa Uganda wanaendelea na uchunguzi wa vifo hivyo.

Vifo hivyo vinadaiwa kutokea Siku ya Jumamosi na Jumapili ambapo miongoni mwa watu waliolazwa hospitalini ni mfanyabiashara aliyekuwa anauza pombe hiyo.
Bado haijajulikana viambata vilivyotumika katika kutengeneza pombe hiyo, iliyochanganywa na maji yasiyo na madini pamoja na ladha ya mananasi.
Msemaji wa jeshi la polisi mkoani humo amesema kuwa sampuli za pombe hiyo zimekusanywa na zitawasilishwa kwa mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya kufanya vipimo.
Washukiwa wanne wamewekwa mbaroni na kiwanda kilichokuwa kinatengeneza pombe hiyo kimefungwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi.
Mwaka 2010, takriban watu 80 walifariki katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Uganda, baada ya kunywa pombe yenye sumu aina ya Methanol.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao