×

Jini mweusi – 60

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Nyuma ya kila kitu, kuna mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, tena akiwa ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, (DCP) Dickson ndiye ambaye anafanya mauaji hayo pasipo kugundulika.

Kazi yake ni kununua machangudoa na yeyote atakayemgundua, humuua kikatili na kuondoka zake. Polisi wanachanganyikiwa, wanamtafuta muuaji, wanamkosa kwani anaonekana makini hasa kwenye kufuta alama za vidole vyake.

Hali ya hofu inaendelea kutanda jijini Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kichwa chake kilifikiria harakaharaka juu ya kile alichotakiwa kufanya mahali pale. Polisi waliendelea kuupiga mlango kwa mateke wakimtaka aufungue lakini hakutaka kufanya hivyo. Kwa haraka sana akaondoka na kurudi chumbani, huko, akachukua kofia yake, akaivaa, akachukua simu yake, kilichofuata ni kuondoka mahali hapo.

Hakupitia mlango wa mbele, alikwenda nyuma ya gesti ile, alipouangalia mlango wa kutokea, ulikuwa umefungwa, dalili zilionesha kwamba haukuwa ukitumika.
Hakutaka kujiuliza juu ya kitu gani alitakiwa kukifanya, akauparamia ukuta, akarukia upande wa pili na kuondoka zake. Hakutaka kusimama sehemu yoyote ile, aligundulika kiulaini kitu kilichomfanya kuwa na hofu kubwa.

Njiani, alipishana na watu, alikutana na vigodoro vya uswahilini lakini hakutaka kusimama, alichokitaka ni kuelekea nyumbani kwake ambapo huko asingekaa sana, angeondoka zake ili kuyaokoa maisha yake.
“Nataka unipeleke Masaki…” alisema mara baada ya kukuta bodaboda njiani.
“Elfu saba…”

“Wewe twende…”
Njiani alikuwa na mawazo mengi, kichwa kilimuuma sana, moyo wake ulijawa hofu, mbele yake aliiona aibu kubwa. Aliwaona Watanzania wakisoma magazeti yaliyokuwa na taarifa yake kwamba yeye ndiye alikuwa muuaji, ndiye yuleyule aliyewaua wanawake na kuitelekeza miili yao na mwingine kumzika msituni.

Aliogopa, aliumia moyoni na wakati mwingine akaanza kujuta. Bodaboda ile haikuchukua muda mrefu ikafika maeneo ya Masaki alipokuwa akiishi, akateremka na kuelekea ndani, huko, akachukua vitu vya muhimu na kuondoka zake. Hakujua aelekee wapi, alichokitaka ni kujificha, ikiwezekana, aende hata katika Kisiwa cha Ukerewe, huko aliamini asingepatikana na angeishi kwa amani kabisa.
* * *
Polisi wakafanikiwa kuuvunja mlango ule na kuingia ndani. Moja kwa moja dada yule akawapeleka katika chumba alichochukuwemo Dickson, walipofika, hawakumkuta zaidi ya kuona maiti ya mwanamke ikiwa kitandani.

Polisi mmoja akaisogelea na kupeleka mkono wake shingoni kuona kama alikuwa akipumua, alitulia kabisa, pumzi ilikata hali iliyoonesha tayari mwanamke yule alikuwa amefariki dunia.

“Ni nani aliyefanya hivi?” aliuliza polisi huku akimwangalia dada yule.
“Kamanda Dickson…”
“Una uhakika?”
“Ndiyo! Nilimuona alipoufungua mlango…”

“Hebu twende kituoni, wewe ni shahidi namba moja…” alisema polisi yule, wakamchukua na kuelekea naye kituoni.
Huko, msichana yule akaanza kusimulia kilichotokea tangu Dickson alipoingia ndani ya gesti ile tena akitangulizana na Happy aliyeonekana kuwa changudoa. Hakuacha kitu, aliwasimulia mpaka aliposikia kelele na kwenda huko ambapo aliambiwa hakukuwa na tatizo.

“Inawezekana kweli?” aliuliza polisi mmoja.
“Ngoja tuwasiliane na Inspekta Maswi kwa ajili ya kuturuhusu kufanya jambo,” alisema kamanda huyo na kuanza kuwasiliana na Inspector General of Police (IGP)
* * *
“Wewe msichana unataka nini hapa?”
“Nimekuja kumuona mpenzi wangu…”
“Nani?”
“Anayeishi humu!”
“Una uhakika anaishi humu?”
“Ndiyo! Huwa ninakuja na kulala naye, kwanza wewe nani mpaka uniulize maswali yote hayo?”

Yalikuwa ni majibizano kati ya msichana Pamela na mwanaume aliyekutana naye nje ya nyumba ya kamanda Dickson. Kwa kumwangalia mwanaume huyo, alikuwa na sura ya kipole lakini alikuwa mtu hatari sana.

Alikuwa miongoni mwa polisi waliotumwa kwa ajili ya kuhakikisha ulinzi wa kutosha unafanyika nyumbani kwa kamanda Dickson kwani tangu polisi hao wapewe na IGP Maswi jukumu la kumfuatilia kamanda Dickson, hawakuweza kumpata zaidi ya kukutana na vielelezo vilivyoonesha kwamba yeye ndiye alikuwa muuaji.

Polisi yule aliyevalia nguo za kiraia akamsogelea Pamela, msichana huyo akabaki akitetemeka, hakujua mwanaume yule alikuwa nani na alihitaji nini kutoka kwake.
“Upo chini ya ulinzi…” alisema mwanaume huyo.
“Chini ya ulinzi nimefanya nini? Wewe ni nani?” aliuliza Pamela, alionekana kuchanganyikiwa.

“Twende kituoni, tunahitaji kuzungumza nawe,” alisema mwanaume yule huku akitoa kitambulisho chake, hakutaka kumfunga pingu Pamela, akaanza kuongozana naye kwenda kituoni.

Njiani, msichana huyo alikuwa akiomba msamaha, hakujua kosa lake lakini kuomba kwake msamaha, aliona kama angeachiwa huru na kuendelea na maisha yake. Alijuta moyoni, kitendo cha kutembea na Dickson ndicho kilichomfanya siku hiyo kuwa chini ya ulinzi.

Mara baada ya kufika katika kituo kikuu cha polisi, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kimoja kilichoandikwa mlangoni ‘Chumba cha Mahojiano’ na kuwekwa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza moja kubwa.

Chumba kizima alikuwa peke yake, alitetemeka kwa kuogopa, baada ya dakika kadhaa, mlango ukafunguliwa, mwanaume mmoja aliyeonekana kuwa hatari, akaingia, mkononi alikuwa na karatasi, sura yake tu ilionesha kuwa ni mtu asiyetaka utani hata mara moja. Pamela akazidi kuogopa.
Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

1 Comment

Leave a Comment