
KLABU ya soka ya Chelsea ya nchini Uingereza imemtia kitanzi mlizni wake wa kulia Reece James kwa kumpatia mkataba mnono wa miaka sita (6) unaotarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Katika mkataba huo Reece James anatarajiwa kupokea kitita cha paundi laki mbili na nusu ambayo ni zaidi ya pesa za kitanzania milioni 500 kwa wiki, kiasi hicho cha pesa kinamfanya kuwa beki anayelipwa pesa nyingi zaidi kuwahi kutokea katika historia ya klabu
Reece James ambaye ameripotiwa kuvivutia vilabu vikubwa Barani Ulaya ikiwemo Real Madrid na Manchester City amezima fununu zote za kuondoka klabuni hapo ikizingatiwa pia kuwa James ni zao la Academy ya klabu hiyo.
Mmiliki mwenza wa klabu hiyo Todd Boehly amesema:
“Tunajisikia Faraja kumpatia James Mkataba mpya na mrefu, ni mchezaji mzuri n ani mtu wa Chelsea na tuna tarajia kumuona akiendelea kufanya vizuri hapa Stamford Bridge.”

Kwa upande wake James amenukuliwa akisema:
“Nimefurahi sana na mkataba wangu na natoa shukrani kwa mashabiki wa Chelsea, Uongozi pamoja na kila mtu anayehusika katika klabu hii, na naimani tutapata mafanikio makubwa pamoja, nimekua nikiwa shabiki wa klabu hii na nimekuwa hapa tangu nikiwa na umri wa miaka sita (6).”
Imeelezwa kuwa baada ya kukamilisha dili la kumuongezea Reece James mkataba mpya, mchezaji anayefuatia ni Mason Mount ambaye naye kama James amekulia katika Academy ya klabu hiyo.