
UWANJA wa Mkapa leo mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya KMC unatarajiwa kuchezwa huku kila timu ikitamba kuwa itafanya kweli kwa kusepa na pointi tatu muhimu.
Simba ambao jana walitangaza kusitisha kibarua cha kocha wao mkuu, Zoran Maki, watashuka uwanjani wakiwa chini ya Kocha Msaidizi, Selemani Matola.
Simba itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi mbili mfululizo kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold na ule wa pili walishinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, wakati KMC wao walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union na sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Polisi Tanzania.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha wa Simba, Matola alisema kuwa wanakutana na timu ngumu ambayo ni KMC lakini wataingia kwa hesabu za kupata pointi tatu.

“Mechi yetu dhidi ya KMC ni ngumu lakini tunakwenda kupambana nao katika kupata pointi tatu, unaona kwamba ushindi wa mechi zetu bila kujali nani anafunga hilo ni muhimu na wachezaji wote wapo tayari isipokuwa Joash Onyango hayupo kwenye mpango wetu kwa kuwa hakufanya mazoezi hivyo masuala yake uongozi unajua namna itakavyokuwa.
“Kwa makosa ambayo tulifanya kwenye mechi za kirafiki limempa nguvu mwalimu kujua namna tutakavyokuwa, tunahitaji pointi tatu muhimu na tutacheza mpira wetu wa burudani, mashabiki wajitokeze kwa wingi,” alisema Matola.
Mohamed Hussein, Nahodha Msaidizi wa Simba alisema wataongeza umakini kwenye safu ya ulinzi ili wawape nguvu washambuliaji kufunga mabao mengi zaidi.
“Tunataka kucheza na kuzuia kufungwa hasa kwa upande wa ulinzi, hiyo itawapa nguvu washambuliaji kufunga kwa kuwa watakuwa wanaona namna ambavyo tunapambana na yeyote anaweza kufunga,” alisema Hussein.
Ahmed Ally, Kocha Msaidizi wa KMC aliliambia Championi Jumatano kuwa, makosa waliyofanya kwenye mechi mbili zilizopita watafanyia kazi ili waanze kushinda mbele ya Simba.
“Tunajivunia kuwa na mshambuliaji mzawa ambaye ameanza kasi katika kufunga na sasa tunakwenda kukutana na Simba tunawaheshimu wapinzani wetu na tunachokitaka ni pointi tatu tukiwa tumeshafanyia kazi makosa yetu,” alisema Ally.
Waandishi: NASSORO MWEMA, HUSNA SOLA, ANGEL MBUNDA, MAPETE IDDI