
Rais wa Kenya Wiliam Ruto ametangaza baraza lake la mawaziri hii leo, wiki mbili baada ya kuapishwa kuwa rais.
‘’Ninajivunia kuwatangazia wanaume na wanawake ambao watahudumu katika Baraza la Mawaziri, Ni muhimu tuunde Baraza jipya la Mawaziri mapema ili tuweze kusimamia kwa haraka masuala ya nchi yetu na kuanza mchakato wa kutekeleza mpango huo’’ alisema Ruto.
Rais William Ruto ameteua wanasiasa mbalimbali kutoka muungano wa Kenya kwanza ikiwemo kigogo wa siasa na aliyekuwa makamu wa rais wa Kenya, Musalia Mudavadi kuwa Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri, mojawapo ya nyadhifa mpya iliyotangazwa.
Rais Ruto aidha amewateuwa wanawake sita kushikilia nyadhifa mbalimbali zikiwemo, wizari za Utalii, Utumishi wa umma na jinsia, maji, afya, ulinzi wa kazi na jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mawaziri wengine aliowateua ni Wizara ya Ulinzi ambayo itaongozwa na Aden Barre Duale, wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora itashikiliwa na Alfred Mutua na wizara ya Afya itaongozwa na Susan Nakumincha Wafula
Mapema leo Ruto alikutana na baraza la mawaziri la serikali iliyopita ya Uhuru Kenyata.