
MSAFARA wa wachezaji 23, benchi la ufundi la watu 8 na viongozi 7 wa AL Hilal ya Sudan wanatarajiwa kuwasilini Tanzania, kesho majira ya saa 12:05 jioni.
Wapinzani hawa ya Yanga SC kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wataondoka Lubumbashi, Congo kesho saa 8:45 mchana wakitumia shirika la ndege la Air Tanzania.
Al Hilal wanatokea Congo walipoweka kambi ya siku 6 kwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Don Bosco na AS Vita Club, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea mchezo dhidi ya Yanga SC
Akizungumza Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu ya Yanga, Saad Kawembwa amesema Uongozi umeshafanya maandalizi yote kwa ajili ya kuwapokea wageni wao.
“Kila kitu kinakwenda vizuri mpaka sasa. Na jambo zuri ni kwamba tuna mawasiliano mazuri na wenzetu mpaka sasa. Kama Klabu tumejiandaa kuwapokea na tutawapa ushirikiano mzuri wakati wote watakapokuwa Tanzania,” alisema Kawembwa
Mchezo wa Yanga dhidi ya Al Hilal utachezwa Jumamosi saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar Es Salaam.