×

John Bocco: Tunawachapa De Agosto Kwao leo Kwenye Uwanja wa 11 de Novembro

KITAPIGWA leo ambapo Simba SC chini ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda, watakuwa Angola kupambana na wenyeji wao, Clube Desportivo 1º de Agosto.

 

Sio kazi nyepesi kutokana na wenyeji kuhitaji ushindi jambo litakaloongeza ugumu kwenye kete ya leo kwa wawakilishi wetu wa Tanzania.

 

Kumbuka huo ni mchezo wa kwanza hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu hatua ya makundi.

 

Baada ya mchezo wa leo ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa 11 de Novembro uliopo eneo la Talatona nchini Angola, marudiano ni wikiendi ijayo Uwanja wa Mkapa, pale Temeke jijini Dar es Salaam.

 

Nahodha wa Simba, John Bocco ambaye kwenye mabao manne iliyofunga timu hiyo dhidi ya Nyassa Big Bullets hatua ya awali, yeye akiwa ametupia bao moja, ameliambia Spoti Xtra kuwa wapo tayari kwa mchezo huo wa ugenini.

 

“Kila mmoja yupo tayari kwa mechi zote ambazo tutacheza, mashabiki tunawashukuru na wazidi kutuombea kwa Mungu tupate ushindi.

 

Mnatarajia ushindani utakuwaje kwenye mchezo huo?

“Tunajua kwamba ushindani ni mkubwa, tunakwenda kufanya kazi ya kusaka ushindi, ambacho tunahitaji ni dua kutoka kwa mashabiki wetu kwani kila timu ambayo tunakutana nayo kwenye hatua za kimataifa tunajua kwamba nao wanahitaji ushindi.

 

“Wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kimataifa, baada ya mchezo wetu wa ligi tulianza maandlizi na sasa tunakwenda kucheza mchezo mgumu ugenini, tunakwenda kukutana na timu nzuri na ngumu.

 

“Timu ambayo imefika hatua hii ambayo sisi tupo tunaamini ni nzuri na ngumu walimu wametupa mbinu na tunakwenda ugenini kutafuta matokeo mazuri ili kurahisisha kazi kwenye mchezo tutakaocheza nyumbani.

 

Mnawatambua wapinzani wenu?

“Kikubwa ambacho tunajua ni kwamba tumepewa mbinu kuhusu wapinzani wetu, benchi la ufundi limewachambua wapinzani wetu na tunajua kwamba nao pia wametuchambua, hilo sio jambo geni.

 

“Tunakwenda ugenini tukiwa tunajua kwamba wao watakuwa nyumbani, benchi la ufundi limejaribu kutueleza mapungufu ya wapinzani wetu.

 

“Siku zote tunajua kwamba mtu anayecheza nyumbani anakuwa na nguvu zaidi, lakini sisi ni timu kubwa, tunakwenda kujituma ili kuiwakilisha timu yetu vizuri pamoja na nchi kwa jumla.

 

Kuna utofauti na mechi za ndani?

“Mchezo wa kimataifa ni tofauti kabisa na mechi za ndani, lakini haya ambayo tunapitia ni somo kwetu na tuna wachezaji ambao wana uzoefu.

 

“Ugumu upo tukiwa ugenini kwamba wapinzani wetu watakuwa wanahitaji kumaliza mchezo wakiwa kwao, lakini sisi tuna imani tutapata matokeo mazuri.

 

Kuna ahadi ambayo mmepewa?

“Klabu imeweka malengo na sisi ni waajiriwa, tupo kwa ajili ya kutimiza malengo ya klabu. Klabu yetu inataka kuona hatua ambayo tulifikia msimu uliopita tunafika mbali zaidi.

 

“Kwa mfano kama wakati uliopita tuliishia robo fainali, basi wakati huu tunahitaji kufika nusu fainali ama fainali, hiyo itakuwa nzuri zaidi.

 

“Hatuchezi kwa historia kwa sababu hatuamini kwamba historia ambayo tulifanya inaweza kujirudia.

 

Vipi kuhusu ahadi ambazo huwa mnapewa mkishinda?

“Huo ni utaratibu ambao huwa unakuwepo, hivyo kama utakuwepo ninaamini kwamba viongozi watatusaidia katika suala hilo,” anamaliza Bocco.

Leave a Comment