
KAGERA Sugar wameiwekea mtego Yanga SC kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika mtego huo, endapo Yanga ikiupita salama, basi itakuwa na asilimia kubwa ya kwenda kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Wakati timu hizo zikiwa zinakwenda kupambana leo Jumapili, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ametamba kutibua rekodi ya Yanga ya kucheza mechi 45 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, huku akibainisha kwamba, wapinzani wao wasije na matokeo ya Waarabu, kwani wataumia.

Akizungumza na Spoti Xtra, Maxime alifunguka kwamba: “Nawapongeza Yanga kwa kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa kimataifa ambao wengi walijua tayari wameondolewa.
“Mbali na hilo, wanapaswa kutambua kuwa mechi yao na Waarabu imepita na sasa wanakuja kukutana na Waswahili wenzao.
“Kwa upande wetu tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye mchezo huu ambao utaendelea kutusogeza kwenye nafasi nzuri.
“Yanga hawajapoteza mchezo wowote kwenye ligi na wapo kileleni kwenye msimamo, hivyo tunaingia kwenye mchezo huu kwa kuwaheshimu, lakini hatuna hofu yoyote, malengo yetu ni kuibuka na ushindi na kutibua rekodi yao ya kutopoteza mechi nyingi kwenye ligi.”
Kagera Sugar hawakuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu hali iliyoufanya uongozi wa klabu hiyo kuachana na kocha mkuu, Francis Baraza na mikoba yake kukabidhiwa Maxime.
Timu hiyo inakwenda kucheza dhidi ya Yanga iliyotoka kushinda 0-1 ugenini nchini Tunisia dhidi ya Club Africain katika mchezo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika na kutinga makundi ya michuano hiyo.
STORI: HUSSEIN MSOLEKA