×

Tulivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi – 3

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nilianza kutetemeka wakati ardhi ikizidi kuzama, ilikuwa kama tupo kwenye lifti na tunashushwa chini kutoka ghorofani, swali likawa tunazamishwa na nani na je tutapona au mwisho wa yote ni kufunikwa na ardhi? Niliwalaumu wenzangu kimoyomoyo kwa kutofuata masharti ya bustani ile ya Mianzi ya Nangose.
Je, huo ndiyo mwisho wa vijana hao?

SONGA NAYO…

Ajabu ni kwamba pamoja na ardhi kuendelea kuzama, sikusikia sauti yoyote kuonesha kuna mashine inaendesha kipande kile cha ardhi kukipeleka chini zaidi ya ardhi.

Kwa kuwa saa yangu ilikuwa inatoa mwanga kwenye giza nene, niliiangalia nikagundua kuwa sasa ni saa mbili tukizama ardhini, sekunde kama kumi hivi nilianza kuona mwanga unajitokeza ukitokea chini ya ardhi.

Nilihisi kwamba tutatokea kwenye ardhi nyingine ambayo hata hivyo sijui kama ni mauzauza au kitu gani.Niliangalia kwa makini nikagundua kwamba bado nilikuwa ndani ya bustani ya Mianzi ya Nangose na mwanga ule hafifu ulioanza kujitokeza ulinifanya niwaone wenzangu wote kuwa bado walikuwa hawajarejewa na fahamu.
Nilikuwa na wazo lingine kabisa kuwa inawezekana wenzangu walifariki dunia wakati mimi nikiamini kuwa walikuwa wamezimia.

Woga ukazidi kunipanda, nikaamua nimsogelee mwenzetu mmoja aliyekuwa karibu na pale nilipokuwa nimeketi kuona kama anapumua au tayari ameshafariki dunia.
Nilikuwa sijawahi hata siku moja kumgusa mtu aliyefariki dunia, sasa nilikuwa sijui anakuwaje. Lakini nikakumbuka simulizi za wazee kwamba mtu akishapoteza uhai mwili wake unakuwa baridi.

Nilimgusa mwenzangu yule na kukuta mwili wake una vuguvugu, hivyo nikaamini kwamba hakufariki. Nilikumbuka kitu kingine, kumgusa kwenye mshipa mkubwa unaopeleka damu kichwani. Kweli nilisikia mapigo ya moyo wake kwa kuhisi kwa mikono kuwa damu inatembea kupelekwa kichwani.

Nilimtikisa huku nikimuita jina “Hamadi, Hamadi, Hamadiii,” akawa kimyaa.
Nilimsogelea msichana mmoja anayeitwa Helena naye nikafanya kama nilivyofanya kwa Hamadi. Nilijaribu kumuita, haikusaidia kitu.

Mkononi mwangu nilikuwa na saa yenye uwezo wa kuonesha muda hata kwenye giza, yaani mishale yake ilikuwa inatoa mwanga, ilinionesha kuwa tangu tuanze kuzama chini ya ardhi tumeshatumia saa tatu. Nilipigwa na butwaa nisijue la kifanya.

Mwanga ulikuja ghafla na kujikuta tupo katika dunia nyingine. Baadaye nilisikia ardhi tuliyokuwa juu yake ikigonga kama vile huko chini yake kuna bati ikawa kama bustani imetua ardhini lakini ajabu ni kwamba kulikuwa na mwanga wa kutosha na tulionekana kama vile tupo juu ya dunia mpya!

Dakika chache baadaye tulishtukia tukiwa tumezungukwa na wanaume wenye ndevu ndefu ambao waliwapulizia dawa wenzangu waliozirai, wakazinduka wote, wakashangaa zaidi yangu kuona tulikuwa dunia nyingine!

Tulipangwa mstari mmoja na kuamriwa kutembea, hatukujua tunapelekwa wapi, wasichana tuliokuwa nao walikuwa wakilia kwa woga!
Japokuwa nilijikaza niliwaangalia wale watu wenye ndevu ndefu waliokuwa wakitusimamia. Tulipangwa mistari miwili na tukaambiwa kuwa tunakwenda kwa mfalme wa nchi ile.

“Tunakwenda kufanya nini?” Niliingiwa na ujasiri nikahoji.
“Ina maana nyinyi ni mataahira. Hamjui kosa hadi sasa?” mmoja wa watu wale aliyekuwa akionekana kama kamanda wao alisema.

“Tunaomba utusamehe,” alidakia kijana mwingine.
“Hakuna kusamehewa hapa. Unajua umetumia nini kufika huku?” akasema yule kamanda.

“Hatujui, kwani huku ni wapi?” niliuliza tena.
“Huku ni nchi ya Ntukuruku.”
Kimyaa kilitanda kwa sekunde kama tano hivi na tukabaki kuangaliana, Nilikuwa najiuliza nchi ya Ntukuruku ni nchi gani? Nilijitahidi kujikumbusha Jiografia, sikumbuki kama kuna nchi yenye jina hilo niliwahi kukutana nalo katika kusoma kwangu.

“Nisiwafiche, nitawaambia kosa lenu.”
“Tafadhali kamanda usitufiche, tuambie nini kosa letu hadi tukaletwa nchi hii ya chini ya ardhi?”
“Wakati mnaingia kwenye bustani ile ya Mianzi ya Nangose, hamkuambiwa miiko?” alihoji kamanda yule.

“Tuliambiwa,” nikajibu.
“Sasa kama ni hivyo, kwa nini hamkutii?”
Kimyaa.
“Nawauliza kwa nini hamkutii?”
“Hatukujua,” alijibu kijana mmoja.

“Hamkujua wakati mlijulishwa kuwa pale nidhamu inatakiwa.”
“Tunaomba sana utusamehe, hatutarudia tena. Sisi tulidhani ni utani tu.”
“Utani? Unaweza kutaniana na mtu mzima kama mzee Mavaka anayetunza bustani ile?”
“Kweli ilikuwa kama anatutania.”

“Hamna adabu kabisa. Kwenu mnataniana na mzee mkubwa kama yule? Hamna hata chembe ya adabu. Mnastahili kabisa kupelekwa kwa mfalme ili iwe fundisho.”
Kutoka pale ‘tulipotua’ na bustani ya mianzi hadi kwa mfalme ni mwendo mrefu. Tulitembea kwa nusu saa na sikuona dalili ya kufika. Tulizidi kuingia kwenye misitu minene yenye miti mikubwa na majani mengi ya kijani.

Moyoni nilikuwa najiuliza kama tutakuwa salama. Nilihisi tunakwenda kuuawa. Njia tuliyokuwa tunapita ilikuwa na alama ya matairi ya magari lakini hatukuona gari lolote likitupita.

Baadaye kwa mbali tukaona watu wengi sana walikuwa wamekusanyika huku wakipiga ngoma na wengine wakiimba.

Hatukuzielewa nyimbo zile zilikuwa na maana gani kwa kuwa walikuwa wakiimba kwa lugha ambayo hatukuijua. Kijana mmoja ambaye alikuwa nyuma yangu nilimhoji kama anaelewa chochote maana ya maneno yaliyokuwa yakiimbwa na watu wale, akasema hajui.

Hata hivyo, kijana mwingine ambaye alikuwa mbele yangu alisema anaelewa lugha hiyo. Nilimuuliza ni lugha gani wanatumia akasema ni Kimeto.
“Kimeto?”

“Ndiyo hicho ni Kimeto, lugha moja inayotumika Kaskazini ya Msumbiji.”
“Wanasema nini?”

“Wanasema hawa ni waharibifu, mfalme wape adhabu kali, ikibidi wafe.”
“Kha! Wanataka kutuua? Hawa watu mbona wakatili sana.”
Tulikaribia jumba la mfalme, tulimuona akiwa amesimama kwenye lango kuu.
Je, nini kitafuata? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave a Comment