
MASTAA wa Simba kesho wanatarajiwa kukwaa kisiki kingine kwa kumenyana na Azam FC ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utapigwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mchezo huo ni kisiki kwao kwa kuwa ule wa mzunguko wa kwanza walinyooshwa bao 1-0 na mtupiaji akiwa ni Prince Dube na wametoka kupoteza mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca.
Azam FC wao walipata muda wa siku 13 kufanya maandalizi kwa ajili ya mchezo huo na walianza rasmi Februari 8, kufanya maandalizi ya mchezo huo na kesho inagota siku ya 13.
Simba walikuwa kwenye maandalizi ya mechi za kimataifa ambapo Februari 18 wamecheza dhidi ya Raja na jana Februari 19 walitarajiwa kuanza maandalizi kuelekea mchezo wao wa kesho.
Kally Ongala, Kocha Mkuu wa Azam FC alisema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Simba wataingia kusaka pointi tatu.
Roberto Oliveira, Kocha Mkuu wa Simba alisema kuwa kwa mechi zote za ligi watafanya maandalizi mazuri ili kupata matokeo.
Stori: Lunyamadzo Mlyuka