
WINGA wa Yanga, Bernard Morrison kwa mara ya kwanza amefunguka suala lake la kukaa nje kwa muda mrefu ambapo amebainisha kuwa tatizo ambalo linamfanya kuwa nje ni la muda mrefu licha ya watu kuona hajaumia katika mchezo wowote.
Morrison amekaa nje kwa muda mrefu na mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa katika mchezo dhidi ya Azam FC, Desemba 25, mwaka jana ambapo Yanga walibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Mghana huyo yuko nje kwa miezi miwili ambapo amekuwa akisumbuliwa na tatizo la nyonga.
Akizungumza kuhusiana na kushindwa kucheza kwa muda mrefu ndani ya Yanga, Morrison alisema kuwa licha ya watu kuona hajaumia katika mchezo wowote lakini alikuwa na tatizo la muda mrefu ambalo ni chanzo cha yeye kukaa nje kwa muda mrefu lakini muda si mrefu atarejea kukipiga huku akiweka wazi kuwa anaipenda timu hiyo.
“Yanga bado naipenda sana watu wanauliza kuhusiana na mimi kutokuumia katika mchezo wowote, nataka tu niwaambie kuwa nilikuwa na tatizo hili kwa muda mrefu jambo ambalo limenifanya niwe nje kwa sasa.
“Mimi bado ni mchezaji halali wa Yanga na nitaendelea kucheza Yanga kwa kuwa bado nina mkataba wa kuitumikia Yanga hivyo muda ukifika nikipona nitaendelea kuipambania Yanga.
“Malengo ya timu ni yale yale kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri katika michuano ya kimataifa na ligi kuu kwa ujumla, nafurahi kuona timu inafanya vizuri naamini nitakuja kuongeza ubora huko mbeleni,” alisema Morrison.