
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakutubi Tanzania, Dr. Leontine Nkebukwa ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) amesema chama hicho kimejikita kuweka misingi imara itakayochochea ari na hamasa ya kusoma au kupata maarifa kupitia uwepo wa maktaba katika ngazi zote.
Miongoni mwa mikakati ya chama hicho ni kuhakikisha maktaba zinaongeza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ambapo pia wameandaa mkutano mkuu na mafunzo ya siku tano yatakayotolewa na chama hicho kuanzia Februari 20 hadi Februari 24, mwaka huu mkoani Tanga..
Aidha ameeleza kuwa maktaba za vyuo zimejikita katika matumizi ya kanzi data mbalimbali ambazo zina vitabu na machapisho mbalimbali.
Dr. Nkebukwa pia amesema Chama cha Wakutubi ili kutimiza azma hiyo kimelenga kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa wakutubi ili kuongeza uwezo katika kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Aidha, chama kupitia wataalamu wake kimeshatoa mafunzo ya kuanzisha kanzi data za taasisi, kuandika miswada ya miradi mbalimbali ya kuendeleza shughuli za tehama katika maktaba, kufundisha njia bora za kufanya tafiti na kusambaza matokeo ya tafiti hizo.
Pia, chama kimeendelea kuiomba serikali kupitia waajiri nchini kuwapa fursa wakutubi wao kuhudhuria semina na makongamano yanayaandaliwa na chama hicho kwa ajili ya kuwaweka wakutubi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Dr. Nkebukwa pia ameomba serikali kupitia wizara ya elimu kuongeza bajeti ya kufufua au kuboresha maktaba za shule za sekondari na za msingi ambazo baadhi hazina wakutubi, vitabu na vifaa vya kisasa vya maktaba.
Makamu mwenyekiti huyo amekumbusha kuwa serikali siku za nyuma ilishaanza mchakato wa kufufua maktaba hizo zoezi ambalo litaenda sambamba na kuajiri wataalumu ambao wapo wengi mtaani bila kazi.
Aidha Dr. Nkebukwa amebainisha kuwa kila mwaka vyuo vya ukutubi hutoa wahitimu wengi ambao hubaki na utaalamu wao mtaani.
Pia Dr Nkebukwa ameishukuru serikali kupitia taasisi za vyuo vya elimu ya juu kuendelea kutoa fedha kuendeleza maktaba kwenye taasisi hizo pamoja na kusomesha wakutubi katika ngazi za uzamivu, uzamili, shahada na stashada.
Aidha, Dr Nkebukwa alimalizia kwa kuwaomba waajiri wa taasisi za serikali na binafsi kulipia wakutubi wao kwa wingi ili waweze kuhudhuria mkutano mkuu na mafunzo ya siku tano yatakayotolewa na chama hicho kuanzia Februari 20-24 mkoani Tanga.