
KAZI kubwa inatarajiwa kufanyika leo Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar ikiwa ni Dabi ya Mzizima kati ya wenyeji Simba dhidi ya Azam FC.
Unakuwa ni mchezo wa pili wababe hawa kukutana katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya ule uliopita wa mzunguko wa kwanza ubao kusoma Azam FC 1-0 Simba.
Katika mchezo wa leo, kila mmoja anataka kushinda ili kuweka heshima, Simba wakitaka kulipa kisasi, Azam kuendeleza ubabe wao.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu, lakini watapambaba kupata ushindi.

“Haitakuwa kazi rahisi katika mchezo huu ukizingatia kwamba tumetoka kupoteza mchezo dhidi ya Raja Casablanca.
“Ninapenda kuona namna ambavyo wachezaji wanacheza, uwezo mkubwa na vipaji vipo, hivyo tutaingia kwa mpango mzuri wa kutafuta pointi tatu na kila kitu kitakuwa sawa, mashabiki waendelee kuwa pamoja nasi,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.
Ofisa Habari Msaidizi wa Azam FC, Hasheem Ibwe, alisema wanatambua ni Dabi ya Mzizima ambayo itakuwa ngumu ila wapo tayari kwa mapambano.
“Kukutana na Simba ikiwa imetoka kupoteza dhidi ya Raja Casablanca ni faida kwetu na hasara pia kwa kuwa wao wataingia na hasira za kimataifa, tutapambana kupata matokeo mazuri,” alisema Ibwe.
Nyota wa Azam FC, Sospeter Bajana, alisema kuwa wanatambua uimara wa wapinzani wao na tahadhari zote wamezichukua.
“Tunaingia kwa tahadhari kubwa kwa ajili ya mechi hiyo na tupo tayari kwa ajili ya mechi zote zijazo, tunachohitaji ni kupata pointi tatu muhimu,” alisema Bajana.