×

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-28

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas aliposema kufuatia mwanaye kufariki dunia alivyotumia muda mwingi kulia na kusababisha usiku huo kutolala. Je, kilifuatia nini baada ya kutokea kwa msiba huo? Songa mbele na mkasa huu wa kuhuzunisha…

Kulipokucha na majirani kukusanyika, yule bwana aliyekuwa anapenda kuniita mjomba, alishauri mama atumiwe taarifa kuhusiana na msiba wa mwanangu.
Hata hivyo, akina babu wawili walisema ni sawa lakini walishauri mwanangu azikwe siku ileile kwa sababu alikuwa bado mdogo hivyo hakukuwa na ulazima wa kumsubiri mama.

Pilikapilika za mazishi ziliendelea na ilipofika saa sita, alikuja mtumishi wa Mungu ikafanyika ibada ya mazishi na mwanangu kuzikwa.
Baada ya msiba baadhi ya akina mama waliniuliza historia yangu lakini sikutaka kuwaambia ukweli zaidi ya kuwafahamisha mama yangu alifariki dunia na kwamba alikuwa rafiki wa mama wa Shinyanga.

Waliponiuliza kuhusu baba wa mtoto wangu, niliwadanganya kwamba kulikuwa na kijana alinirubuni na kunipa ujauzito kisha kutoweka ndipo mama akaamua kunipeleka kule kijijini kwa bibi.

Akina mama hao walihuzunishwa na taarifa niliyowapa ambapo yule mama niliyekuwa napenda kwenda kwake alinipa moyo kwamba kila binadamu hukumbana na mitihani hivyo nisihuzunike sana.

Mama huyo aliongeza kuniambia, kikubwa ni kujifunza baada ya kukosea awali ili nisirudie tena kosa.Alipotoa kauli hiyo niliumia sana moyoni kwa sababu tangu nilipojitambua nilikuwa makini ila Evance ndiye aliyeniingiza kwenye matatizo baada ya kunibaka.

Hata hivyo, sikuwa na jinsi zaidi ya kumshukuru Mungu na kupanga kuondoka kule kijijini kwa njia yoyote na kurudi mjini ambapo pia nilipanga nisingekaa ningeenda Mbeya kwa mama mkubwa.

Kila nilipokumbuka maisha ya upendo niliyoishi nilipokuwa na marehemu mama na mama mkubwa wa Mbeya, nilijuta kwa nini nilikubali kwenda kuishi Shinyanga.
“Kama ningekuwa Mbeya kwa mama mkubwa, wala nisingebakwa na kupata mimba na kutelekezwa huku kijijini kama vile sina thamani,” nilijikuta nikiwaza.

Wiki moja baada ya msiba wa mwanangu sikuona sababu ya kuendelea kuishi kule kijijini, siku moja usiku nikiwa nimeketi na bibi nilimwambia anipatie nauli ili nirudi mjini.

Bibi aliniambia kwamba nisubiri mpaka mama atakapokuja, kauli yake ilinitibua nikamweleza kwa kitendo cha mama kunitelekeza kule bila msaada wowote sikuwa na sababu ya kumsubiri.

Licha ya umri wangu mdogo, nilimwambia bibi mwanaye alikuwa mtu mbaya sana na kumwuliza kama mjukuu wake Emmy ndiye angekuwa alipewa mimba angefanya kama alivyonifanyia?

Kumtetea mwanaye, bibi aliniambia kwa anavyomfahamu mama akufanya vile kwa makusudi isipokuwa alihisi kuna jambo lilimbana hivyo nisimuwazie vibaya.
Nilimweleza hata kama angekuwa kabanwa hakunitendea haki kunipeleka kijijini huku akijua nilikuwa mjamzito, afadhali hata kama angemtuma mama mdogo aje kuniangalia lakini wote hawakufanya hivyo.

Baada ya kuzungumza mengi na bibi, nilimwomba anitafutie nauli hata kwa kukopa kwa majira zake ili niende mjini, akaniambia nisubiri kukicha atanipa jibu.

Asubuhi bibi aliniaga kwamba anatoka kidogo ambapo alirejea kwenye saa tatu hivi akaniambia alizungumza na mtu mmoja aliyemuahidi kumpatia fedha jioni ya siku hiyo.
Taarifa hiyo ilinifurahisha, nilimsaidia bibi kazi mbalimbali na jioni ilipofika bibi aliondoka tena na aliporejea aliniambia nijiandae kwa safari ya mjini siku iliyofuata.
Nilimshukuru bibi, usiku huo niliweka nguo na vitu vyangu kwenye begi tayari kwa alfajiri kuanza safari, bibi aliponiuliza kama ningeweza kufika mwenyewe nikamwambia ningefika.

Kulipokucha, bibi alinisindikiza hadi sehemu ya kupandia magari tukakuta Canter moja ikiwa imejaza watu na mizigo, nami nikapanda ambapo hatukukaa sana safari ikaanza.
Tulisafiri kwa muda mrefu ndipo tuliingia Shinyanga mjini, kwa kuwa nilikuwa mwenyeji niliposhuka kwenye gari nikabeba begi langu na kuanza kuelekea nyumbani.
Njiani watu waliokuwa wakinifahamu walinishangaa na kuniuliza mbona nilibadilika sana, badala ya kuwajibu nikaanza kulia.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

Leave a Comment