Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.
Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Nyuma ya kila kitu, kuna mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, tena akiwa ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, (DCP) Dickson ndiye ambaye anafanya mauaji hayo pasipo kugundulika. Kazi yake ni kununua machangudoa na yeyote atakayemgundua, humuua kikatili na kuondoka zake.
Polisi wanachanganyikiwa, wanamtafuta muuaji, wanamkosa kwani anaonekana kuwa makini hasa kwenye kufuta alama za vidole vyake. Hali ya hofu inaendelea kutanda jijini Dar es Salaam.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Pamela alibaki akitetemeka pale kitini, kila alipomwangalia mwanaume yule aliyeingia, hakuonekana kuwa na utani, muonekano wake tu ulionesha kwamba alitaka kuambiwa ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea, vinginevyo asingeweza kueleweka.
Mwanaume huyo akakaa kwenye kiti na kuweka zile karatasi juu ya meza, macho yake akayatuliza kwa Pamela ambaye tayari kijasho chembamba kilianza kumtoka huku kwa mbali akitetemeka kama mtu aliyeanza kuhisi baridi kali.
“Unamfahamu huyu?” aliuliza mwanaume yule huku akimuoneshea Pamela picha ya Kamanda Dickson, yaani hata kumsalimia hakutaka, kwake, maswali yalikuwa muhimu zaidi ya salamu.
“Nd..iy..o..” alijibu Pamela huku akitetemeka.
“Ulishawahi kumuona wapi?”
Hapo ndipo Pamela alipoanza kuhadithia namna alivyokutana na Kamanda Dickson tangu siku ya kwanza mpaka siku ya mwisho kuachana naye. Katika kipindi chote hicho cha kuhadithia, mwanaume yule alikuwa kimya akimsikiliza, pale alipoona kulikuwa na jambo la muhimu kuandika, aliandika kwenye moja ya karatasi zake.
“Ulishawahi kumuuliza kwa nini alikuwa akificha sura yake siku za kwanza?” aliuliza mwanaume yule.“Hapana! Sikutaka kujali sana kwa kuwa nilihisi kwamba yeye ni mume wa mtu hivyo hakutaka kugundulika, sikuwa na hofu, nilichokiangalia ni fedha tu,” alijibu Pamela.
“Unahisi kwa nini aliwaua wanawake aliokuwa akiwachukua?”
“Nahisi walimgundua. Hata siku ya kwanza nilipouona uso wake akaniuliza kwa nini sikushtuka au kuogopa? Kwa kuwa sikuwa namfahamu, nikamwambia siwezi kushtuka wala kuogopa. Nahisi wale waliomgundua ndiyo aliowaua kwa kudhani siri yake ingegundulika,” alisema Pamela.
Kila swali aliloulizwa mahali pale, alijibu kiufasaha kabisa. Mahojiano hayo yalichukua zaidi ya dakika thelathini ndipo akaruhusiwa kuondoka huku akiambiwa kwamba alitakiwa kufika pale kituoni kila atakapokuwa akihitajika.
* * * *
Watu walijaa katika meza za wauza magazeti, walichokuwa wakikiona, hawakukiamini hata kidogo. Minong’ono ya hapa na pale ilikuwa ikisikika katika kila meza ya magazeti iliyokuwa imekusanya idadi kubwa ya watu.
Habari iliyokuwa imeandikwa katika magazeti hayo, ilimshtua kila mmoja, hakukuwa na aliyeamini kwamba mtu aliyekuwa akiwaua wanawake wale katika kipindi chote hicho alikuwa Kamanda Dickson, mtu aliyeheshimika na kuogopwa mno na wahalifu.
Hiyo ndiyo ikawa habari ya mjini, kila gazeti lililokuwa na habari hiyo, lilinunulika na mpaka kufikia saa sita mchana, hakukuwa na gazeti lolote mitaani lililokuwa na habari kuhusu Kamanda Dickson.
Habari hiyo haikuwa peke yake bali hata uthibitisho wa picha ya gari lake likiwa nje ya gesti moja Mwananyamala ilisindikizia habari hiyo kitu kilichowafanya watu wengi kuamini kwamba kamanda huyo ndiye alikuwa muuaji wa wanawake wale.
“Mimi siamini mwenzenu…” alisikika mwanamke mmoja aliyesimama mbele ya meza moja ya magazeti.
“Wewe ndiyo kama mimi! Eti Kamanda Dickson muuaji, sasa huku kuchafuana kumezidi, kwanza magazeti haya bora yafungiwe tu,” aliisema mwanaume mmoja aliyeonekana kukasirishwa mno na habari hiyo.
“Kwanza haya magazeti yafungiwe kwa kumchafua kamanda wetu, mchapakazi na anayejitolea sana, pili ni lazima jeshi la polisi liingilie kati, haiwezekani lichafuliwe kiasi hiki tena kwa habari ya kuungaunga kama hii,” aliingilia mwanaume mwingine, kila mtu aliyekuwa mahali hapo alionekana kukasirishwa na habari ile.
Mijadala iliendelea mitaani, watu walikuwa wakibishana kwamba inawezekana habari hizo zilikuwa ni za kutengenezwa kwa ajili ya kumchafua mtu fulani. Japokuwa ukweli uliandikwa gazetini lakini hakukuwa na mtu aliyeuamini, kila mmoja alihisi kwamba taarifa hizo zilikuwa kwa lengo la kumchafua kamanda huyo.
Taarifa hazikutolewa gazetini tu, ilipofika saa saba mchana, karatasi zenye picha zake zikaanza kubandikwa katika vituo mbalimbali vya daladala, mitaani kwamba Dickson alikuwa mtu hatari na yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake basi kitita cha shilingi milioni ishirini kingekuwa kama zawadi yake.
Hapo ndipo wale watu ambao hawakuamini kilichoandikwa magazetini wakaamini. Hoja zikaibuka tena, mijadala ikaanza kwenye mitandao ya kijamii, watu wengi walikuwa wakilishutumu jeshi la polisi kwa kutokulivalia njuga suala hilo mpaka pale wanawake wengi walipouawa.
“Polisi wazembe sana…” alilalamika jamaa mmoja pasipo kukumbuka kwamba mtu aliyekuwa akifanya mauaji alikuwa Kamanda Mkuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kila mtu alizihitaji hizo milioni ishirini. Kumgundua Kamanda Dickson halikuwa jambo gumu, alijulikana kila kona, ubaya wa sura yake ulikuwa gumzo. Watu wakawa makini mitaani, wengi waliokuwa hata wakifanana naye walichukuliwa na kupelekwa kituoni.
Siku ya kwanza ikapita, wananchi walikuwa makini kila kona lakini hawakuweza kumpata. Siku ya pili ikaingia, ya tatu mpaka ya nne lakini bado polisi na wananchi waliendelea kumtafuta pasipo mafanikio.
Wakati polisi wakiendelea kumtafuta kwa kufuatilia hata akaunti zake benki, wakagundua kwamba siku moja nyuma, kiasi chote cha fedha alichokuwa nacho kilihamishwa na kupelekwa katika akaunti ambayo hawakuiona, walishindwa kufahamu ni nani aliyefanya hivyo na fedha hizo zilikuwa katika akaunti ya nani.
Kama fedha zilihamishwa kisiri, ilimaanisha kwamba alikuwa sehemu. Yeye hakuwa na utaalamu wa masuala ya kompyuta, je ni nani aliyemsaidia kuhamisha fedha hizo pasipo benki kujua mahali zilipopelekwa? Mbali na hiyo, je, huyu Kamanda Dickson alikuwa wapi? Hilo ndilo swali alilojiuliza kila mtu pasipo kupata jibu.
Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.