×

Serikali Yatoa Msimamo Vita ya Sudan, Mapigano Yasimama Kwa Saa 24 -“Hakuna Mtanzania Aliepata Madhara”-Video

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stergomena Tax.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stergomena Tax amesema hakuna Mtanzania aliyepo Sudan aliyepata madhara kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Amesema wapo Watanzania takribani 210 nchini Sudan na kwamba serikali imekuwa ikiwasiliana mara kwa mara na ubalozi wa Tanzania jijini Khartoum kuhakikisha Watanzania hao wanakuwa salama.

Hayo yamesemwa mapema hii leo Aprili 19, 2023 Bungeni na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Stergomena Tax.

Waziri Tax amesema Tanzania inasikitishwa na hali ya kuzorota kwa amani nchini Sudan kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya jeshi na wapiganaji wa kikosi cha RSF.

“Serikali imeendelea kufanya mawasilano ya mara kwa mara na ubalozi wetu uliopo mjini Khartoum, ili kujua hali inavyoendelea. Tunao Watanzania takriban 210 nchini Sudan ambapo 171 kati ya hao ni wanafunzi, na wengine ni maafisa wa ubalozi na raia wengine. Hadi sasa hakuna Mtanzania aliyeripotiwa kuathiriwa na mapigano hayo. Namshukuru balozi wetu kwa kuhakikisha usalama wa raia wetu nchini humo.”

Wakati huo huo, amesema serikali inawahakikishia Watanzania kwamba inachukua hatua stahiki kwa kushirikiana na nchi jirani, jumuiya za kikanda, Umoja wa Afrika, na Umoja wa Mataifa, na taasisi nyengine za kimataifa ili kuhakikisha kuwa Watanzania waishio nchini humo pamoja na raia wengine wapo salama.

Baadhi ya wanafunzi waliopo nchini Sudan wamesema kwamba tangu kuanza kwa mgogoro huo mbali na changamoto za kiusalama, pia kumekuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na hata wakati mwengine kuzimwa kwa mtandao wa Internet.

Hali ya wasiwasi pia imetanda miongoni mwa wazazi, ndugu na hata marafiki ambao mpaka sasa hawajui hatma ya ndugu zao waliokwama nchini Sudan tangu kuibuka kwa vita hivyo.

Hivi sasa matumaini pekee yaliyopo ni iwapo zuio la mapigano la saa 24 litafanya kazi na kuheshimiwa na pande zote hasimu.

Leave a Comment