×

The angel of darkness – 39

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari na kuacha gumzo kubwa jijini Arusha, wanasafiri mpaka kwenye Visiwa vya Hawaii kula fungate. Wakiwa kwenye fungate, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego.

Anaificha siri hiyo moyoni mwake na kumfanya Msuya aamini kwamba ni mimba yake. Baada ya kukaa mwezi mzima Hawaii, wanarudi Arusha ambapo Arianna anamwambia Diego kwamba ana mimba yake, mwanaume huyo anachanganyikiwa mno.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Diego hakuamini alichokisikia kutoka kwa Arianna kwamba ule ujauzito aliokuwa nao ulikuwa wake. Akamwangalia msichana huyo kwa macho yaliyojaa maswali mengi yaliyochanganyikana na mshtuko mkubwa.

Alimpenda sana msichana huyo, alimthamini katika maisha yake, alikuwa tayari kwa lolote lakini kuambiwa kwamba ule ujauzito ulikuwa wa kwake, hilo lilimchanganya kupita maelezo.
“Unasemaje?”

“Kwani hukunisikia?”
“Nilikusikia, ila inawezekana sikukuelewa….”
“Nimesema hivi, huu ujauzito ni wako,” alisema Arianna huku akilishika tumbo lake.
Diego hakutaka kubaki pale kochini, akasimama na kuanza kutembea-tembea sebuleni, japokuwa kulikuwa na kiyoyozi kilichokuwa kikipiga lakini kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Moyo wake ulikuwa na hofu kubwa, alimfahamu mzee Msuya, alionekana kuwa mpole sana lakini kila alipoyaangalia macho yake, hakuonekana kuwa mpole kama alivyohisi, bali inawezekana alikuwa mzee katili, asiyehofia kutoa uhai wa mtu hasa kwa aliyemletea mchezo kwa msichana aliyekuwa akimpenda.

“Haiwezekani…” alisema Diego huku akirudi kochini.
“Haiwezekani nini?”
“Wewe kuwa na mimba yangu…hiyo si mimba yangu,” alisema Diego huku akimwangalia Arianna usoni.

“Diego…”
“Nini?”
“Mimi ni nani kwako?”
“Dada yangu…”
“Dada yako? Unajifanya umesahau mimi ni nani?” aliuliza Arianna, alionekana kuanza kubadilika.

“Sawa, mpenzi wangu, ila mpenzi anayenitesa kila siku…” alijibu Diego kwa sauti ya chini.

“Kama mimi ni mpenzi wako wa siri, jua hii ni mimba yako.”
Diego akabaki kimya. Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, aliyahofia maisha yake, kama ambavyo msichana huyo alivyosema kwamba ule ujauzito ulikuwa wake basi hata pale ambapo mtoto angezaliwa, ilikuwa ni lazima kufanana naye kitu ambacho kingesababisha kuwa mwisho wa maisha yake.

“Ni lazima tufanye kitu, ninaogopa huyu mzee akigundua kwamba hiyo mimba ni yangu,” alisema Diego.
“Ila nina uhakika hatajua…”
“Lakini kumbuka utajifungua, mtoto akifanana na mimi unafikiri nini kitafuata? Sitaki kulipuliwa kwa mafuta ya petroli ni lazima uitoe hiyo mimba,” alisema Diego huku akimwangalia msichana huyo.

Arianna akashtuka, hakuamini kusikia kile alichokisikia kutoka kwa mwanaume huyo. Alimwangalia Diego mara mbili-mbili, maneno yake yalimchanganya kichwa chake.
Kuutoa ujauzito ule kilikuwa ni kitu kisichowezekana hata kidogo, aliyahofia maisha yake kwa kuwa utoaji wa mimba haukuwa na uhakika wa kuwa hai asilimia mia moja.
“Kutoa mimba? Hapana…” alisema Arianna.

“Arianna, ninaogopa, utanisababishia niuliwe, naomba utoe hiyo mimba hata kwa kunywa vidonge na useme mimba imeharibika, la sivyo huyu mzee ataniua…” alisema Diego.

Kwa jinsi alivyozungumza kipindi hicho hata Arianna mwenyewe akabaki akimshangaa, hakuamini kama Diego huyu, mwanaume mkorofi ambaye kila siku alijitapa kwamba hakuogopa kitu chochote kile leo hii alikuwa mpole namna hiyo.

Sauti yake ilitoka kipole, tena ya kuomba mno, hata macho yake yalionyesha ni jinsi gani alimtaka msichana huyo kuutoa ujauzito huo, ila pamoja na hali zote hizo, msimamo wa Arianna ulikuwa uleule, mimba haitolewi.

“Kwa hiyo upo tayari kuniona nikiuawa?” aliuliza Diego.
“Na wewe upo tayari kuona nikifa wakati natoa mimba yako?” naye Arianna aliuliza swali.

Diego hakujibu swali hilo, alinyamaza na kusimama tena. Hakutaka kuendelea kubaki sebuleni pale, akaelekea chumbani kwake ambapo huko alijilaza kitandani na kuanza kufikiria mambo mengi.

Wakati mwingine moyo wake ulikuwa na majuto tele, alijuta kwa kitendo chake cha kutembea na msichana Arianna na wakati tayari alipata maisha mazuri ambayo hakutegemea kuyapata na hata hakufikiria kama ingetokea siku angepata maisha kama aliyeokuwa akiishi kwa mzee Msuya.

Huo haukuwa muda wa majuto tena, jambo lililokuwa mbele yake ni namna ambavyo angeweza kulitatua tatizo kubwa lililojitokeza kwani suala la kutoa ujauzito ule tayari Arianna alilikataa katakata.

“Ni lazima tutoroke mahali hapa,” alisemaDiego.
Huo ndiyo uamuzi aliokuwa ameufikia, hakutaka kuendelea kuishi ndani ya nyumba ile kwa kuamini kwamba maisha yake yote yangekuwa yenye kujaa hofu ya kuogopa kuuawa, hivyo kitu alichokifikiria ni kutoroka pale, si peke yake bali pamoja na Arianna.
Aliporudi sebuleni, akamkuta msichana huyo mahali hapo, hakutaka kusubiri, akaanza kumwambia mpango alioufikiria kwamba ili kuepuka kifo na mateso makali kutoka kwa mzee Msuya, ilikuwa ni lazima watoroke.

“Tutoroke?” aliuliza Arianna.
“Ndiyo!”

“Hicho ni kitu kisichowezekana hata kidogo…yaani nimtoroke mume wangu! Hapana,” alisema Arianna huku akionekana kumaanisha alichokisema.
“Arianna….”
“Nimesema siwezi kutoroka…siwezi kuondoka kwa mume wangu…”
“Ila nitauawa, naogopa ukijifungua mzee Msuya atagundua…”
“Nisikilize Diego, nimesema hivi…siwezi kutoroka..”
“Nakuo…..”

“SIWEZI KUTOROKA…” alisema Arianna kwa sauti kubwa.
Diego akachanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya kumshawishi msichana huyo.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatatu katika Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave a Comment