LIPOISHIA WIKIENDA
“Sawa. Mimi nilikuwa nakushauri tumfungulie akaunti mtoto wetu kwa ajili ya maisha yake ya baadaye. Wewe mwenyewe hujui utakuwa waziri hadi lini.”
Aliponiambia hivyo nilishindwa kujizuia kucheka.
“Mbona unanicheka, au nimetoa wazo baya?” akaniuliza.
“Ni wazo zuri lakini ni mapema mno kumfungulia akaunti huyu mtoto, bado ni kichanga sana.”SASA ENDELEA…
“Inatakiwa awe na miaka mingapi?”
“Angalau afikishe miaka minne.”
“Miaka minne, si tutakuwa tuna mtoto mwingine?”
“Haijalishi, bado tunaweza kumfungulia akaunti.”
Mazungumzo na mke wangu yaliponoga tukahamia sebuleni. Nikawa nimeshasahau kuwa nilikuwa nimekasirika.
Tulikuwa tukizungumza huku tukicheka. Mke wangu alikuwa mjanja sana.
Siku iliyofuata niliamka mapema alfajiri nikatoka uani na kuuchukua ule mkoba wangu, nikaenda kuuficha katika chumba cha stoo.
Muda wangu wa kwenda kazini ulipowadia nikatoka kwenda zangu kazini.
Ilipita kama miezi tisa hivi, nikaanza kuona vituko. Ikumbukwe kwamba wale wazee wachawi wa kule kwetu Nzega nilikuwa nimewapuuza na sikuwa na mawasiliano nao. Hata nilipokwenda Nzega kukutana na wapiga kura wangu sikuwa nikifika kwao.
Nilikuwa bado nakumbuka siku ile waliponiadhiri mbele ya watu katika mkutano wangu kwa kuniambia kuwa nilikuwa mchawi mwenzao. Bahati njema watu walipuuza maneno yao na hakukuwa na aliyewatilia maanani.
Pia nilikuwa nakumbuka nilivyowaamuru polisi wawakamate wakasweka ndani ambapo usiku wake walitoroka kimiujiza kwa kujigeuza paka.
Kitendo chao kile cha kutaka kuniadhiri mbele ya watu ndicho kilichonifanya niwapuuze. Lakini nikajua, hatua yangu ya kuwaamrisha polisi wawakamate iliwatia hasira dhidi yangu.
Baada ya miezi tisa tangu mke wangu ajifungue mtoto, usiku mmoja wakati tumelala, nilishtuka usingizini nikasikia kama vishindo vya watu nje ya dirisha.
Nilitega masikio yangu ili nisikilize kwa makini kile nilichokuwa nakisikia, nikahakikisha kwamba kulikuwa kumeingia watu waliokuwa wakiizunguka nyumba yangu.
Nikaisikia waziwazi sauti ya mzee Mgorozi ikisema:
“Tumefuata mtoto wetu…tumefuata mtoto wetu…”
Kauli ile ikanishtua. Nikamtazama mke wangu kujua kama alikuwa macho, nikashukuru kugundua kuwa alikuwa amelala. Kama angekuwa macho na angesikia yale maneno ingekuwa patashika na nguo kuchanika.
Hapo ndipo nilipogundua kuwa hilo lilikuwa kundi la wachawi kutoka Nzega. Bila shaka walikuwa wamesafiri kwa nyungo kunifuata Dar.
Kile kimya chao cha muda mrefu kilinidanganya nikadhani waliamua kuachana na mimi kwa vile nilikuwa siwajali, kumbe walikuwa wameishika ile ahadi niliyowapa kwamba nitawapa mtoto wangu wa kwanza wamle.
Kusema kweli ingawa nilitoa ahadi hiyo lakini sikuwa tayari kumtoa mtoto wangu aliwe na wachawi hao.
Nilikumbuka vizuri kwamba babu yangu aliniambia kwamba alitakiwa na wachawi hao anitoe mimi. Akadai kuwa hakuwa na mtu mwingine wa kumsaidia zaidi yangu.
Hivyo akawaahidi wanisubirishe nizae mtoto. Mtoto wangu wa kwanza watamchukua badala yangu.
Wachawi hao walikubali kwa sababu mimi mwenyewe pia nililazimishwa na babu kurithi mikoba yake ya uchawi, hivyo wachawi hao wakaniona ni mwenzao.
Pia niligundua ilikuwa kawaida kwa wachawi wa kwetu kuwatoa kafara watoto wao au wajukuu zao.
Sasa kwa vile na mimi nilijiunga katika kundi hilo, wajibu huo wa kutoa mtoto kafara ukanipata.
Sikujua kama wachawi hao walikuwa wakifuatilia nyendo zangu. Na pia sikujua kama wangejua nimepata mtoto bila kuwafahamisha mimi mwenyewe. Na ndiyo maana niliishi bila wasiwasi nikijua mwanangu sitamsaliti na atakuwa salama. Kumbe haikuwa hivyo.
Baada ya ile sauti ya mzee Mgorosi, zikasikika sauti zingine zikiwemo za wanaume na wanawake zikisema hivyo hivyo.
“Tumefuata mtoto wetu…tumefuata mtoto wetu…!”
Nyumba niliyokuwa ninaishi ilikuwa inalindwa na mlinzi saa ishirini na nne, lakini niliamini kuwa alikuwa haoni kilichokuwa kikiendelea kwani watu hao waliingia mle ndani kiuchawi.
Nikamtazama mwanangu Mkanga aliyekuwa akilala kwenye kitanda chake kilichokuwa karibu na kitanda chetu upande aliolala mama yake. Nikamuona yupo. Nikainuka na kwenda kumuondoa kwenye kitanda chake na kumlaza sehemu ya katikati ya kitanda chetu kisha na mimi nikalala.
Laiti kama ningekuwa na bunduki ningetoka nayo na kuwatimua wachawi hao.
Kama ningepiga risasi moja juu nilikuwa na hakika kwamba wangekimbia. Lakini sikuwa na bunduki. Ikabidi ninyamaze kimya.
Licha ya sisi kuwa kimya, wachawi hao waliendelea kuizunguka nyumba yangu huku wakitamka yale maneno kuwa wanamtaka mtoto wao.
Kusema kweli nilikosa amani na nilikuwa nikiomba mke wangu asiamke na kuzisikia zile sauti.Wasiwasi ulinipata nilipomuona Mkanga akitikisika kama aliyesisimka kisha akajigeuza upande mwingine.
Nikaweka mkono wangu kifuani mwake.
“Huyu haendi popote” nikajisemea kwa sauti ya taratibu. “Sitakubali achukuliwe hata iweje.”Zile sauti zilipozidi, nilitamani nitoke niwafukuze lakini nilishindwa kwani nilijua walikuwa wamejiandaa kupambana na mimi.
Ghafla nikaona kundi hilo limekuja dirishani mwa chumba tulichokuwa tumelala na kudai kuwa wanamtaka mtoto wao. Nikapata hofu kuwa mke wangu ataamka.