×

Mkuki Moyoni Mwangu – 14

HALI ya Catarina imeimarika na ameruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea nyumbani furaha kati yao ikitawala kwa wazazi wa pande zote mbili.Wanaongea mengi juu ya maisha yao huku wakiwaomba wazazi wao wawape ruhusa ya kufanya kile alichokitamani maishani mwao jambo ambalo wazazi wanalikubali kwa asilimia zote.

Jambo hilo linamfanya Kevin kutabasamu, hakuwahi kuwa na furaha maishani mwake kama kipindi hicho, aliamini kila kilichotokea kuanzia ajali yake, kuugua kwa Catarina kilimaanishwa kuwaunganisha wao badala ya kuwatenganisha, ilikuwa rahisi sasa kwa wazazi wao kukubaliana na kitu walichoomba kwa sababu ya mapito magumu waliyopitia.Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

HALI ya Catarina iliendelea kuimarika, akipewa dawa za kuua bakteria, dawa za fangasi kupambana na madonda mdomoni na kwenye njia ya chakula yaliyojitokeza sababu ya kupungukiwa kinga mwilini na pia chupa za damu ziliendelea kuongezwa mwilini mwake.

Kwa mwezi mzima aliendelea kubaki wodini na Kevin muuguzaji wake, waliongea mengi kuhusu maisha, wote wakila kiapo cha kutokutana na mwanamke au mwanaume kimwili mpaka watakapotimiza ndoto yao ya kuoana na kuzaa watoto, Catarina aliendelea kusisitiza nia yake ya kuwa mwanamitindo maarufu duniani, hiyo ndiyo kazi pekee aliyotamani kuifanya wakati Kevin ndoto yake iliendelea kubaki kuwa Mhandisi, tofauti na kazi ya udaktari ambayo baba yake alitaka aifanye maishani.

Familia zao zilishaunganishwa, urafiki kati ya wazazi wao ulikuwa mkubwa mno, walijiona ni ndugu wakiwa tayari kwa lolote ambalo watoto wao wangetaka kulifanya. Catarina aliruhusiwa kutoka hospitali wiki ya tano tangu awekewe Uboho, Saratani ya damu ikiwa imepimwa na kuonekana haiko mwilini mwake na kurejea nyumbani kwao Victoria ambako walihamia na wazazi wake baada ya kutokea mgogoro siku za nyuma.

Wazazi wake hawakuona tena sababu ya kuendelea kuishi hapo, wiki moja baadaye waliamua kurejea kwenye nyumba yao ya awali, kuishi tena wakiwa majirani na familia ya Kevin, ilikuwa ni furaha kubwa mno kwa watoto hao kukaribiana kama mwanzo, ukizingatia sasa uhuru kati yao ulikuwa mkubwa.

Sherehe kubwa ya kumshukuru Mungu ilifanyika na majirani pamoja na marafiki wakaalikwa, baba wa Catarina alitangaza siku hiyo kwamba yeye na mzee Mdoe walikuwa Pacha, jambo lililoashiria kwamba familia hiyo sasa ilikuwa imeunganishwa na kuwa moja.

“Hii ina maana utakuwa dada yangu?” Kevin alimuuliza Catarina.
“Hata simuelewi baba.”
“Hakuna cha udada na ukaka hapa, wewe ni mke wangu tu!”
“Hayo mengine watayajua wenyewe.”
“Kabisa.”

Mwezi mmoja baadaye utaratibu wa kuwarejesha shule ulianza kufanyika, Catarina hakutaka tena kwenda nchini Uganda ingawa Kevin alikubali kurejea St. Joseph, lakini kurudia kidato alichokuwa kabla ya kuugua. Wazazi wa Catarina walimtafutia nafasi katika Shule ya Sekondari ya Marian Girls iliyoko Bagamoyo mkoani Pwani, iliyosifika kwa kufaulisha wanafunzi kuliko shule nyingine yoyote mkoani humo.

Kama ilivyokuwa kwa Kevin, Catarina pia alirudia darasa alilokuwa akisoma kabla ya kuugua, wakatenganishwa na elimu tena! Lakini mioyo yao haikuwauma kama ilivyokuwa mwanzo kwa sababu sasa kulikuwa na uelewano mkubwa kati yao na familia zao.

Shule zilipofungwa walikutana nyumbani na kuendesha maisha yao kama marafiki, wakitunza kiapo walichojiwekea cha kutokukutana kimwili mpaka ndoa, Catarina hakuwa na matatizo kabisa kiafya, vivyo hivyo Kevin, kufahamu kwamba Catarina aliwahi kuugua Saratani ya damu ilikuwa ni lazima upewe historia hiyo na mtu mwingine lakini si kwa kumwangalia.

Familia zao zilishirikiana kwa kila kitu, ikiwemo kusafiri kwenda Mbuga za wanyama za Serengeti wakati wa likizo na tayari walisali kanisa moja la Christ Embassy Mikocheni, wokovu ukiwa umewajaa mioyoni mwao, kila siku wakiwaombea watoto wao wasije wakaingia majaribuni bali mpango wa Mungu katika maisha yao utimie.

Kevin alipomaliza kidato cha nne aliendelea na kidato cha tano katika shule hiyohiyo, lakini kwa upande wa Catarina aligoma kabisa kuendelea na shule akiwa kidato cha nne akidai alikuwa amekutana na Mzungu kutoka Afrika Kusini aliyekuwa akizunguka Afrika kutafuta wasichana ambao wangeweza kufanya kazi ya Uanamitindo.
“Umechanganyikiwa?” Mama yake alimuuliza.

“Sijachanganyikiwa mama, hilo ndilo jambo ninalotaka kulifanya maishani.”
“Uanamitindo? Uache shule kwa ajili ya Uanamitindo kazi ambayo huwezi kuifanya mpaka ukiwa na umri wa miaka thelathini?”

“Najua mama, lakini hapo ndipo moyo wangu ulipo naomba tu uniache.”
“Hapana, suala hili lazima tuliongelee na baba yako na ikibidi tukutane na huyo Mzungu.”

“Nitamleta.”
Kwenye umri wa miaka kumi na tano Catarina alikuwa ni tishio, alisharefuka mpaka urefu wa futi 5 na inchi 8 mwembamba mwenye sura ya Kiethiopia, pua ya Kinyarwanda, shingo ndefu ya Kisukuma, kiuno chembamba cha Kinyarwanda, miguu minene ya Kinyakyusa, hakika kila mwanaume aliyemwona Catarina alimshangaa Mungu kwa uwezo wake wa kuumba, Catarina alikuwa mrembo na kilichomfanya awe mrembo zaidi ni mwanya, pamoja na vishimo viwili kwenye mashavu yake vilivyochombezwa na kidoti cheusi kando ya pua yake ambacho Wazungu hukiita ‘Beauty Spot’

Baba yake alipopewa taarifa hizo kwanza alihamaki, lakini alipoongea na mtoto wake na kugundua kabisa alikuwa amedhamiria na kwamba hata shuleni alikuwa hafanyi vizuri sababu ya kufikiria mitindo, alijikuta hana la kufanya isipokuwa kumwomba amlete nyumbani Mzungu huyo ili wapate kuzungumza naye na kupata uhakika wa usalama wa mtoto wao.

Siku chache baadaye Catarina alitimiza jambo hilo kwa kumleta Mzungu nyumbani kwao, akawahakikishia wazazi ya kwamba mtoto alikuwa katika mikono salama kwa kuwafungulia mtandao wa kampuni aliyokuwa akiiwakilisha ya Fonex Modeling Company SA, pia akawaeleza kuwa kama kampuni walikuwa na utaratibu wa kuwaendeleza watoto kielimu huku wakiendelea kufanya kazi.

Wazazi waliulizia kila kitu juu ya malipo na kuelezwa jinsi mkataba ulivyo iwapo Catarina angepita kwenye vigezo vyote na kuanza kufanya kazi, malipo ya chini kabisa yalikuwa ni dola milioni moja na laki mbili kwa miaka miwili! Zilikuwa ni fedha nyingi mno hasa baada ya baba yake kuchukua mashine ya hesabu na kuzibadilisha kwenda katika shilingi.

“Are you sure she will be safe?” (Una uhakika atakuwa salama?)
“One hundred percent!” (Asilimia mia moja!)
“Then let’s sign the agreement!” (Basi tutie saini mkataba!)
“Give me three days!” (Nipe siku tatu!)

Siku tatu baadaye mkataba ulitiwa saini kwenye ofisi za kampuni ya uwakili ya Law Associates ya jijini Dar es Salaam waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakishuhudia na kutangaza jioni katika taarifa za usiku, siku iliyofuata picha ya Catarina ilikuwa kwenye magazeti yote ukurasa wa mbele chini ya vichwa mbalimbali vya habari vikimsifia.

Wiki moja baadaye ilikuwa ni siku ya ndugu kutembelea wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya St. Joseph, alichokifanya Catarina ni kuongozana na wazazi wake pamoja na wazazi wa Kevin kwenda shuleni kumpelekea Kevin taarifa hizo ambazo hakuna mtu aliyekuwa amempatia, hawakuwa na uhakika angezipokeaje lakini jambo ambalo walijua lingetokea ni kilio.

Tofauti na matarajio yao, Kevin alipopewa taarifa hizo alifurahi na kumuunga mkono Catarina akidai chochote cha kumfurahisha ndicho angetaka kifanyike, furaha ya Catarina ikaongezeka kupita kiasi, akamhakikishia Kevin ya kwamba asingemsahau maishani na kama angefanikiwa lazima angemchukua kumfuata hukohuko.
“Wasiwasi wangu ni mmoja tu.”

“Upi?”
“Catarina umekuwa mzuri sana, matajiri wanaweza kuninyang’anya!”
Kauli hiyo ya Kevin ilimfanya Catarina amkumbuke Craig Anderson, Mzungu mwakilishi wa Kampuni ya Fonex Modeling aliyemgundua na kuamua kumpeleka Afrika Kusini, kuna wakati alimwangalia kwa jicho la mahaba ambalo Catarina hakulielewa vizuri.

“Wala usiwe na wasiwasi, hakuna mwanaume anayeweza kuniondoa kwako!” Catarina aliongea, wakakumbatiana na Kevin kuanza kulia kwa uchungu, kutengana kuliwasikitisha.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave a Comment