
Dar es Salaam 6 Juni 2023:Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) imefanya semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC) kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi.
Akizungumza wakati wa semina hiyo iliyofanyika mapema leo katika Chuo Cha Kodi kilichopo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Makao Makuu, Richard Kayombo amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa wanahabari ili nao waende kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala zima la ulipaji kodi.

Kayombo amesema elimu hiyo ni pamoja na kuongeza ujuzi na kufundisha uelewa wa kulipa kodi ambayo elimu hiyo haitofautiani sana na maswala yaleyale ambayo kila siku unapozidi kujifunza unapata elimu zaidi ikiwa ni lengo kujenga taifa moja.
“Tunapolipa kodi ndio inayojenga taifa kupitia mambo mbalimbali ikiwemo barabara kama mnavyoona siku hizi barabara zimeunganisha mikoa hadi mikoa kwenye hospitali kuna mashine za x-ray siku hizi tofauti na zamani ulikuwa ukiandikiwa kupiga picha ya x-ray ni lazima uende Muhimbili lakini sasa hivi hospitali nyingi za serikali zina mashine hizo na nyinginezo, hiyo ni kutokana na kodi. “Hivyo ndivyo tunavyoweza kujenga taifa na kujiimarisha na kijitegemea kiuchumi.

“Ni wajibu wa kila mlipa kodi kuandikishwa kwa ajili ya kodi pale ambapo sheria za kodi zinamtaka kufanya hivyo, pia ana wajibu wa kuwasilisha ‘ritani’ na kufanya malipo ya kodi kwa wakati kama ulivyowekwa kwa mujibu wa sheria ya kodi,” amesema Kayombo.
Aidha mlipa kodi ana wajibu wa kudhihirisha shughuli zake za kibiashara pamoja na matokeo yake kwa ukamilifu na kwa usahihi, wajibu wa kutoa risiti za kodi kila anapouza bidhaa au anapotoa huduma na wajibu wa kudai risiti za kodi kila anaponunua bidhaa au anaponufaika na huduma iliyotolewa.

Ameendelea kusema kuwa wajibu wa kutoa ushirikiano kwa TRA katika kudhihirisha miamala yake yote ya mapato na matumizi ya biashara kuwasilisha nyaraka na kumbukumbu za biashara zake na yeye binafsi kujitokeza kwa kuja ofisi za TRA, pale atakapotakiwa kufanya hivyo.
Pia amesema malengo ya ukusanyaji kodi ya shilingi Trilioni 23.1 unaendelea vyema na kuwahimiza wananchi kulipa kodi na kujenga taifa.
Kuhusu wanaoingiza bidhaa za magendo kutoka nchi za nje amesema si salama kwa kuwa zinaweza kuleta athari kwani huwa hazijapimwa na kuthibitishwa na mamlaka husika hivyo kuweza kusababisha madhara kwa watumiaji na pengine huenda ikawa ni bidhaa haramu kama vile dawa za kulevya, silaha au vinginevyo.
Hivyo Kayombo amewataka wafanyabiashara kutonunua bidhaa hizo ili kuepuka madhara yatokanayo na bidhaa hizo za magendo.