
MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, jana Jumamosi walifanya gwaride la kusherehekea ubingwa wao wa 29 walioutwaa msimu huu wa 2022/23, huku wakiwatambia wapinzani wao kwa kuwaambia: “Jifunzeni kwetu, sisi ndiyo wakali wa hizi shoo.”
Yanga ambayo ndiyo timu iliyobeba mataji mengi ya Ligi Kuu Bara tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo mwaka 1965 ambayo ni 29, ilifanya gwaride hilo kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar, muda mfupi baada ya kikosi kutua kikitokea Mbeya.

Kikosi hicho kimetoka Mbeya kilipoenda kucheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons na kuibuka na ushindi wa mabao 0-2, Uwanja wa Sokoine, juzi Ijumaa.
WATUA KIBABE
Mashabiki na wanachama wa Yanga, walijitokeza kwa wingi jana uwanja wa ndege mapema tu kuisubiria timu yao kuungana nayo katika shamrashamra hizo ambapo kikosi hicho kilitua majira ya saa 5:59 asubuhi, kisha msafara ukaanza safari saa 6:40 mchana, kuelekea Makao Makuu, Jangwani.
Kumbuka hii ni mara ya pili mfululizo wanafanya gwaride hilo wakiwa na gari la wazi, awali walifanya msimu uliopita 2021/22 walipobeba ubingwa wa ligi hiyo.

MAYELE AZUA HOFU
Baada ya kikosi hicho kutua, mshambuliaji wa timu hiyo, Fiston Mayele, alizua hofu baada ya kuonekana akitembea kwa kuchechemea.
Kutokana na hali hiyo, mashabiki wakaanza kuhofia kumkosa mshambuliaji huyo katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, itakayochezwa kesho Jumatatu dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
MSAFARA WASIMAMA, MAYELE, HERSI WATETEMA
Kutoka Uwanja wa Ndege, msafara huo ulipita Barabara ya Nyerere hadi Tazara, kisha ukakata Barabara ya Mandela hadi Buguruni, ukafuata Barabara ya Uhuru.
Msafara huo ulipofika Ilala Boma, ulisimama kwa muda, kisha Mayele na Rais wa Yanga, Injini Hersi Said, wakaanza kushangilia kwa staili ya kutetema baada ya mashabiki kuomba lifanyike jambo hilo.

VIBAKA WATUMIA FURSA, WADHIBITIWA
Katika mkusanyiko mkubwa, uvunjifu wa amani mara kadhaa hutokea, ndiyo ilikuwa hivyo baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka, walitumia fursa hiyo kufanya uhalifu, lakini walidhibitiwa vikali na wananchi ambao waliwashushia kipigo hadi askari walipoingilia kati na kurudisha amani iliyotoweka kwa muda.
MANARA AIBUKIA MSIMBAZI, AINUA KOMBE KIBABE
Wakati safari inaanza Uwanja wa Ndege, Haji Manara ambaye amefungiwa kwa muda wa miaka miwili kujihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya Tanzania, ilidaiwa hayupo, lakini ghafla akaonekana walipofika Mtaa wa Msimbazi, yalipo Makao Makuu ya Simba SC.
Manara ambaye hadi anafungiwa alikuwa Msemaji wa Yanga, msafara ulipofika Msimbazi, alionekana akiinua kombe kibabe na kushangilia kwa nguvu, huku Mayele akitetema.
MASHABIKI SIMBA WATOE MAKOMBE YAO
Wakati Yanga wakishangilia kwa kuonesha kombe lao walipofika Mtaa wa Msimbazi, mashabiki na wanachama wa Simba waliokuwa Makao Makuu Msimbazi, nao walitoa makombe ambayo timu yao imewahi kuyatwaa, kisha kushangilia.
Simba ambayo msimu huu imemaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara, imewahi kubeba ubingwa huo mara 22, huku mara ya mwisho ikichukua msimu wa 2020/21, ilifanya hivyo mara nne mfululizo kuanzia 2017/18 hadi Yanga ilipokuja kufanya mapinduzi 2021/22 na 2022/23.
STORI NA JOEL THOMAS NA MARCO MZUMBE