
Dar es Salaam 3 Julai 2023: Kutoka katika Viwanja vya Mwalimu Juliaus Kambarage Nyerere (Sabasaba) jijini katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa vijana ambao ni wanafunzi kutoka chuo cha Veta Dodoma, wamenufaika na program ya mafunzo mbalimbali yatolewayo katika chuo hicho.
Moja ya program zinazotolewa katika chuo hicho ni fani ya umeme ambapo mwanafunzi, Patrick Ezekiel ameeleza jinsi alivyonufaika ikiwa yeye akishirikiana na mwalimu wake wameweza kuunda mfumo wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji.

Amesema huo mfumo wameutengeneza ili aweze kujifunza kwa urahisi jinsi umeme unavyozalishwa na namna unavyosafirishwa hadi kufika vituo vya kupozea umeme na kisha kusambaza kwa watumiaji.
“Kitu ambacho tumekifanya katika huu mfumo kunakuwa na jenereta ambayo litategemea kupata nguvu ya mzunguko kutokana na kasi ya maji na pia kutakuwa na transfoma kwa ajili ya kuukuza umeme. Pia kunakuwa na vifaa kwa ajili ya kulinda soketi na vifaa vingine vinavyohitajika kuwepo kwenye transfoma.
“Huu mfumo wa umeme ni namna halisi wa uzalishaji unaotumika katika vituo vyetu hapa nchini hivyo nawaambia vijana waje katika chuo cha ufundi Veta ili waweze kujifunza na kupata maarifa na kujikomboa kiuchumi iwe kwa kuajiriwa au kujiajiri,” amesema.