
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema zaidi ya vijana 800 wanaotarajiwa kuhitimu mafunzo ya BBT mwaka huu wanatarajiwa kunolewa kuhusu masuala ya uzalendo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mkataba wa makubaliano kuhusu mafunzo hayo ya mwezi mmoja yamesainiwa leo na kushuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maonesho ya wakulima Nane nane yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Vijana hao waliokuwa katika vituo atamizi 13 kwa kipindi cha miezi mine, tarehe 20 Agosti mwaka huu wanatarajiwa kukodishiwa mashamba kwa miaka 66 ili kuendeleza shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji baada ya kupatiwa mafunzo hayo.
Amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuwatafutia wawekezaji watakaonunua mazao yatakayozalishwa kwenye mashamba hayo ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba katika mashamba hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesaini hati ya makubalino na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele kwa ajili ya ushirikiano katika kuwaendeleza vijana kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT).