
Jeshi la Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini limetoa elimu kwa viongozi wa Wafugaji toka Mikoa ya Arusha na Manyara wanaozunguka Hifadhi za taifa za Wanyama kuhusiana na namna bora ya kuepuka migogoro ya malisho wakati wa kiangazi.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU) Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua ametoa elimu hiyo mapema leo huko katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire Mkoani Manyara na kuwataka wafugaji kutumia kipindi hiki ambacho hakina ukame kujiandaa vyema na kutenga maeneo ya malisho ambayo watayatumia kipindi cha kiangazi.
Kamanda Pasua amebainisha kuwa Jeshi hilo limeamua kuwatumia Viongozi hao wa Mila maarufu ‘’Legwanani’’ ili wafikishe ujumbe huo kwa jamii nzima ya wafugaji ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara ya kugombania maeneo ya malisho.
ACP Pasua amefafanua kuwa kupitia elimu ambayo imetolewa ni imani yake kuwa hakutakua na migogoro baina ya wafugaji, wakulima lakini pia maeneo ya hifadhi za Taifa.
Kwa upande wake Bwana Julius Mariki toka wilayani Monduli amesema changamoto kubwa waliyonayo wafugaji ni mabadiliko ya hali hewa na tabia nchi ambapo amekiri kuwa hakuna mbadala uliopo zaidi ya elimu kuendelea kutolewa kwa jamii hizo za kifugaji ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya mara kwa mara.