×

Wamiliki wa Vyombo vya Habari Mitandaoni Watakiwa Kutoa Elimu Kuhusu Ulipaji wa Kodi

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja

Wamiliki wa vyombo vya habari vya mitandaoni (online media) wametakiwa kuwa kielelezo katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kulipa kodi na kudai risiti halali yenye thamani halisi ya huduma au bidhaa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja wakati akifungua Kongamano la Wanamitandao ya Kijamii na Wizara ya Fedha linalofanyika Mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia Oktoba 23 hadi 24 , 2023.

“Mitandao ya Kijamii imekuwa nyenzo kubwa ya kuifikia jamii kwa haraka na kwa ukubwa hivyo niwaombe mtumie fursa hiyo kuielimisha jamii umuhimu wa kudai risiti yenye thamani halali ya huduma uliyoipata,” amesema Mwaipaja.

Pia amewataka wanamitandao hao kuisaidia serikali kuielimisha jamii kuhusu agenda ya maendeleo ya taifa na miradi inayotekelezwa na serikali kwa ajili ya maslahi ya Watanzania ikiwemo miradi ya kimkakati.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja

Aidha amewapongeza kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya  kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha katika kuhabarisha umma juu ya mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara hiyo.

“Wizara inawatambua nyie ni wadau muhimu sana katika kutoa taarifa zetu na mmekuwa mkifanya hivyo siku zote na jamii imekuwa ikipata taarifa kupitia mitando yenu bila kuda chochote kwa hilo niwapongeze sana”ameeleza

Katika hatua nyingine, Mwaipaja amewatoa hofu Watanzania kuhusu deni la taifa kuwa linalipika na ndio maana serikali inaendelea kuaminika na inakopesheka kwa manufaa ya Taifa.

“Ukiona mtu anakopeshwa ujue ameaminika na ndio maana mpaka kuna baadhi ya taasisi za nje ya nchi zinaomba zitukukopeshe ama zifadhili miradi yetu kwa hilo tu jamii iamini kuwa nchi ipo salama na deni la taifa bado ni himilivu linalipika,” amesisitiza Mwaipaja

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kongamano hilo, Mathias Canal ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa kongamano hilo la siku mbili litakalowakutanisha waandishi wa habari za mitandao na kusema kuwa hiyo itakuwa fursa ya kurahisisha utendaji kazi wao kwa umma.

Canal ameitaka wizara ya fedha kuhakikisha kuwa inatoa ufafanuzi kwa umma kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali na umuhimu wa mikopo ili kuondoa sintofahamu kwa jamii kuhusu mikopo ya serikali.

Leave a Comment