×

Ushindani wa Masomo Una Faida Zake

Ni vigumu kwa sehemu yoyote kufanya jambo kwa bidii bila kupoteza lengo ikiwa hakuna ushindani. Ushindani baina ya watu wawili wenye lengo sawa mara zote huchochea kasi ya maendeleo.

Kwenye ulimwengu wa kujifunza hali huwa ileile ambapo wanafunzi wanaokuwa na ushindani wa masomo hujikuta wakiongeza ufaulu kwa aidha kufikia malengo yao au kuvuka kabisa malengo yao ya ufaulu kuliko sehemu ambayo wanafunzi hawana ushindani wa aina hiyo.

Ni jambo la kawaida kwa wanafunzi kuwazidi wenzao katika viwango vya ufaulu huku wanafunzi waliozidiwa wakiridhika na hali hiyo kwamba mtu fulani ana uwezo kuliko wao na hawezi kufikiwa kimasomo.

Katika hali kama hiyo wanafunzi wa shule hiyo wanakuwa katika hatari ya kushuka viwango vyao vya kufaulu kwa kuwa pengine anayewaongoza kwenye shule yao hamfikii hata kidogo mwanafunzi anayeongoza kwenye shule yenye ushindani mkubwa wa masomo miongoni mwa wanafunzi.

Hiyo inaweza ikathibitishwa pale ambapo wanafunzi hao watakutanishwa aidha katika mitihani ya kanda au ya kitaifa ambapo utaona hata ufaulu wa wanafunzi wanaoongoza katika shule hizo mbili wanavyotofautiana viwango vya kufaulu.

Kama hiyo haitoshi, hata kwa wanafunzi ambao wanaonekana hawana akili katika shule ambazo zina ushindani huweza kuwapita wenzao ambao hujisomea bila ushindani wa kimasomo.

Kwa mantiki hiyo ni vyema basi wanafunzi wenyewe kwenye shule mbalimbali kuweka ushindani na yule anayewaongoza kwa wastani mkubwa wa kufaulu na kumuwekea malengo ya kumzidi ufaulu kwa njia ya kujisomea pekee na si nyinginezo.

Unaweza ukatangaza ushindani naye kwa kumwambia waziwazi kuwa unataka kumpita mtihani ujao, hii itakufanya usijisahau kufuata ahadi yako huku yeye pia akijitahidi kusoma kwa bidii kwa kuogopa kufikiwa.

Wakati huo unaweza ukajifunza kwa kutazama mwenendo wake wa kujisomea kisha wewe ukazidisha mara nyingi zaidi yake huku ukipima uwezo wako na wake kwa kulinganisha viwango vya ufaulu wenu hata katika majaribio madogo ya awali.

Ni wazi kuwa wanafunzi wengine hawapendi kutoa mitihani yao lakini ushindani huu una faida kubwa kwa wanafunzi wote; wale wenye ufaulu mzuri na wale wasio na ufaulu mzuri darasani.

Wale wenye ufaulu mzuri watakuwa na faida ya kuongeza bidii ya kujisomea ili kuhakikisha hawafikiwi, huku wale wenye ufaulu mdogo wakijisomea kwa bidii zaidi ili kuhakikisha wanampita yule ambaye anawaongoza kila siku.

Ipo mifano hai mingi ya wanafunzi waliojiwekea ushindani wa aina hii wakifaulu vizuri kuliko hata wale walioamini kuwa wana akili kuzidi wao; Jaribu sasa.

Leave a Comment